WAANDISHI WA HABARI REDIO ZA MWANZA, KAGERA, GEITA NA MARA WAPATIWA MAFUNZO YA M - MAMA

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt.  Jesca Lebba akizungumza na waandishi wa habari katika uzinduzi wa semina ya waandishi wa habari wa radio Kanda ya ziwa

Na Mbuke Shilagi Mwanza.

Waandishi wa Habari wa Radio Kanda ya Ziwa wamepatiwa semina ya mfumo wa M-mama ambapo wametakiwa kuelimisha jamii kuhusu mfumo wa M-mama na matumizi sahihi ya namba 115 pindi mama mjamzito, aliyejifungua ndani ya siku 42 pamoja na mtoto mchanga ndani ya siku 28 atakapoona dalili za hatari katika mwili wake atoe taarifa mapema kupitia namba hiyo.

Akizungumza mapema leo Novemba 8, 2024 mgeni rasmi Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Jesca Lebba jijini Mwanza uliohudhuriwa na waandishi wa habari wa Radio kutoka Kagera, Geita,  Mwanza na Mara pamoja na wadau wa Afya amesema kuwa kupitia mfumo wa M-mama tangu umezinduliwa tayari rufaa elfu 98 zimepokelewa ambapo akina mama walikuwa elfu 78 na watoto wachanga elfu 19 wamenufaika kupitia mfumo huo.

"Kama tunavyojua kuwa M-mama ni huduma ya usafiri wa dharura wa kumfikia mama mjamzito, mama aliyejifungua ndani ya siku 42 pamoja na mtoto mchanga ndani ya siku 28 pindi wanapopatwa na dalili za hatari ndani ya jamii au hata katika vituo vya afya ikiwa lengo ni kuondoa au kupunguza kabisa vifo vya mama na mtoto", amesema Dkt.  Jesca.

Aidha amesema kuwa katika mfumo wa M-mama walengwa ni mama mjawazito, mama aliyejifungua mpaka siku 42, mtoto mchanga mpaka siku 28, pamoja na jamii kwa ujumla ikiwa lengo kuu ni kuokoa maisha ya mama na mtoto pamoja na kumuwaishia huduma za kiafya mlengwa huyo.
 
"Serikali ililiona hilo na kuleta mfumo huu wa M-mama ili kusaidia au kuepusha sababu ya pili ya miundombinu na usafiri ili basi kumuwezesha mlengwa kufika kwa wakati katika kituo cha afya na kupatiwa matibabu",

"Naomba tuendelee kuelimisha jamii kupitia mfumo huu kutumika ipasavyo na ninaomba nisisitize mfumo huu kutumika vizuri na wamama wajawazito waache kutumia dawa za kienyeji badala yake wahi katika kituo cha afya na hapo utaokoa mtoto aliye tumboni na maisha yako pia", amesema Dkt. Jesca.













Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post