Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza Nicodemus Tenga, leo Novemba 11, 2024,amepokea msaada wa mifuko 260 ya Saruji yenye thamani ya shilingi milioni 5,070,000 kutoka kwa Maafisa na Askari wa kozi ya kijeshi namba 12 ya mwaka 1994 (Depo).
Hafla ya makabidhiano hayo imefanyika katika viwanja vya Hospitali ya Jeshi la Magereza iliyopo eneo la Msalato jijini Dodoma, ikishuhudiwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Mkurugenzi wa Usimamizi wa Kesi na Utaratibu wa Upelelezi kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Mhe. Saraji Iboru, Genes Tesha pamoja na Aldom Mkini wote kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka.
Akizungumza mara baada ya kukabidhi msaada huo, Mwenyekiti wa Umoja wa Kozi ya Kijeshi namba 12 ya mwaka 1994, Kamishna Msaidizi wa Magereza (ACP) Joyce Mkufya, alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha kwa ajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo katika Jeshi la Magereza.
"Kwa umoja wetu, tumehamasika kumuunga mkono Mheshimiwa Rais Dkt.Samia kwa kununua mifuko ya saruji 260 yenye thamani ya shilingi 5,070,000 na kukabidhi kwa Mkuu wa Jeshi ili isaidie kujenga Maabara katika Hospitali mpya ya Jeshi, tulipata mawazo mengi ya kufanya katika jamii, lakini tukaona ni vyema tuunge mkono juhudi hizo kwa kununua mifuko 260 kwaajili ya kujenga Maabara katika hospitali hiyo ambayo ikikamilika itahudumia makundi mbalimbali katika jamii inayozunguka eneo hili" Alisema ACP. Mkufya.
Kwa upande wake, Mhandisi wa ujenzi wa hospitali hiyo, SSP.Bonanza Malata, aliwashukuru wanajumuiya wa Depo namba 12 ya mwaka 1994 kwa msaada huo, na kusema kuwa saruji hiyo itatumika katika malengo yaliyokusudiwa.
Social Plugin