Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA Ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA,) imezindua rasmi jukwaa la uwekezaji la M-WEKEZA ambao ni mradi wa pamoja wa kampuni ya Sanlam Investments East Africa Limited na M-PESA Limited na kuelezwa kuwa hiyo ni hatua muhimu katika maendeleo ya sekta ya fedha hususani masoko ya mitaji katika ukanda wa Afrika Mashariki.
Akizungumza leo Novemba 21,2024 jijini Dar es Salaam wakati wa kuzinduliwa kwa jukwaa hilo Mkurugenzi Mkuu wa CSMA CPA. Nicodemus Mkama amesema uzinduzi wa jukwaa hilo utaimarisha na kuongeza kasi ya malengo ya kuwawezesha kifedha wafanyabiashara binafsi katika ukanda wa Afrika na kupitia M-WEKEZA jukwaa la uwekezaji kwa njia ya simu litawawezesha watu binafsi kupata fursa ya uwekezaji kwa urahisi katika maeneo ya mijini na vijijini kwa kutoa huduma za kifedha.
CPA Mkama amesema mpango huo unatoa fursa za uwekezaji kwa wawekezaji wakiwemo wanawake na vijana hali itakayochagiza maendeleo kwa kuhamasisha akiba ya ndani kupitia uwekezaji, kutengeneza fursa za ajira na kujenga uchumi thabiti wa Taifa.
“Uzinduzi wa jukwaa hili pia unaendana na mfumo wa tatu wa kitaifa wa ujumuishaji wa kifedha wa 2023/2028 ambao unasisitiza matumizi ya kidigitali katika usambazaji na utoaji huduma za kifedha.” Amesema.
Ameipongeza menejimenti ya Sansalam Investment East Africa Limited na M-PESA Limited kwa jitihada za kuunganisha mifumo yao na kupata kibali cha CMSA ambayo imeendelea kuweka mazingira rafiki ya kisera, udhibiti na utendaji yanayochagizwa na uimara wa Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
"Kazi kubwa ya masoko ya mitaji ni kukusanya rasilimali kutoka kwa wawekezaji na kuzielekeza kwenye uwekezaji wenye tija na kuchochea maendeleo katika Serikali, mamlaka za mitaa, taasisi kubwa na ndogo na kampuni mbalimbali ambazo hutoa fedha zinazoelekezwa katika miradi mbalimbali ya maendeleo,"amesema CPA Mkama.
Social Plugin