Mradi wa ujenzi wa daraja la Mto Kalambo lenye urefu wa mita 80 pamoja na ujenzi wa barabara unganishi ya Sopa- Mtutumbe- Kasitu ni moja ya kielelezo cha jitihada zinazofanywa na Dkt. Samia katika kuleta maendeleo nchini.
Katika mradi huo, Serikali kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA ), imekamilisha ujenzi wa daraja la Mto Kalambo lenye urefu wa mita 80 pamoja na ujenzi wa barabara unganishi ya Sopa- Mtutumbe- Kasitu kwa kiwango cha changarawe, kwa gharama ya Shilingi Bilioni 5.142 katika Halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Mkoani Rukwa.
Meneja wa TARURA Mkoa wa Rukwa, Mhandisi Chacha Moseti ameishukuru Serikali kwa kutoa fedha hizo kwa ajili ya ujenzi wa daraja hilo ambalo limenufaisha Wananchi wa Kata za Sopa na Pombwe, kusafirisha mazao yao sokoni kwa urahisi.
Daraja hili limesaidia Wananchi wanaojishughulisha na kilimo cha Maharage, Mahindi, Alizeti pamoja na shughuli za ufugaji ambao kwa sasa wanasafirisha mazao yao kwenda Sumbawanga na Tunduma bila shida yoyote.
Kukamilika kwa daraja hilo kumerahisisha kuendelea kufanyika shughuli mbalimbali za maendeleo ambapo wananchi wameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutengeneza daraja hilo kwani kipindi cha nyuma wanafunzi walikuwa wanashindwa kuvuka mto huo kwenda shule ambapo kwa sasa wanavuka bila shida na wanafika shule kwa wakati.