MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu,akichagia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mwongozo wa Maandalizi ya Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha wa 2025/2026 leo Novemba 5,2024 bungeni jijini Dodoma.
Na.Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Singida Mashariki Miraji Mtaturu amechangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mwongozo wa Maandalizi ya Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha wa 2025/2026,huku akisisitiza mambo manne ya kuzingatiwa.
Mambo hayo ni ujenzi wa mabweni kwa ajili ya wanafunzi,nyumba za walimu,madaraja na kilimo cha umwagiliaji.
Akichangia mapendekezo hayo Novemba 5,2024,Bungeni Jijini Dodoma,Mtaturu amesema serikali imefanya maendeleo makubwa katika sekta mbalimbali ikiwemo elimu,afya na huduma za wananchi ambapo madarasa,maabara na matundu ya vyoo yamejengwa.
“Maeneo mengi, tumeona maboresho makubwa,lakini kuna changamoto ya mabweni ambayo tunatakiwa tuongeze nguvu kujenga ili watoto wetu waweze kuwa na mazingira mazuri ya kujifunzia,lakini pia tuhakikishe kwamba tunajenga nyumba za walimu ili tuwasaidie wanaokaa mbali na eneo la shule,”.amesema.
Amesema barabara zimejengwa vijijini hivyo maeneo mengi wananchi wanasafirisha mazao yao,wanasafiri kwenda eneo moja hadi lingine lakini bado kwenye madaraja nguvu inahitajika ili wananchi waweze kufurahia mipango ya serikali na kuhakikisha kwamba wanaongeza uchumi wao.
“Pamoja na kuboresha mazingira ya wananchi kufanya shughuli zao,pia tuongeze kilimo cha umwagiliaji ili kuongeza uchumi wa wananchi mmoja mmoja,”ameongeza.
AIPONGEZA SERIKALI.
Ameipongeza serikali chini ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwekeza katika sekta ya miundombinu ya nishati na usafirishaji hivyo kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuchochea uwekezaji chini.
“Nianze kumpongeza Rais Samia kwa kusimamia maono yake na kusimamia mpango wanaoenda kuumaliza wa mwaka mmoja na kuja na mpango mzuri unaoonyesha mwelekeo wa kuweza kuleta maendeleo zaidi katika nchi yetu,kwa hakika katika mwaka mmoja huu tunaomaliza tumefanya kazi nzuri sana na sisi tuliopo majimboni tumeona fedha nyingi zimekuja kutekeleza miradi,sisi wabunge tunampongeza sana,”amesema.
Social Plugin