Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NAIBU WAZIRI SAGINI- MSIKATISHWE TAMAA KATIKA KUPAMBANIA HAKI ZA BINADAMU


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

MTANDAO wa Wanawake Watetezi wa Haki za Binadamu umetakiwa kutokukata tamaa licha ya kupitia kadhia ya vitisho,kutukanwa na kupewa majina mabaya wakiwa katika jukumu lao la mapambano yao dhidi ya udhalimu na dhuluma dhidi ya haki za binadamu.

Hayo yamesemwa leo Novemba 29,2024 Jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Sheria na Katiba Mhe. Jumanne Sagini katika maadhimisho ya kusherekea  siku ya wanawake watetezi wa haki za binadamu ambayo hufanyika Novemba 29 kila mwaka.

Amesema Wizara ya Sheria na Katiba kwa kushirikiana na taasisi zinazohusika na masuala ya haki za binadamu,wanajukumu la pamoja la  kuweka mifumo ambayo itawezesha wanawake hao wanaohusika na utetezi wa haki za binadamu,kufanya kazi yao katika mazingira salama.

"Mmeweza kushawishi serikali kuwa na Sheria zinazotoa usawa wa kijinsia  na kukemea sheria kandamizi dhidi ya wanawake na wasichana,mmechangia pia ushirikishwaji wa wanawake katika ngazi za maamuzi" Amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Mtandao wa Wanawake Watetezi wa Haki za Binadamu,Wakili Maria Matui amesema kuwa bado hakuna mfumo rafiki ambao unamwezesha mwanamke mtetezi kufanya kazi yake bila hofu

"Tumeona bado hakuna mfumo wa kumtetea mwanamke huyu anayewasemea walio wengi ambao hawawezi kujiongelea haki zao"Amesema.

Sambamba na hayo,Wakili Matui ametoa ombi kwa serikali kuunda mifumo itakayomsaidia  mwanamke mtetezi wa haki za binadamu ili kumuweka katika mazingira salama katika utekelezaji wa jukumu hilo.

Nae Mratibu wa Mtandao wa Wanawake Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania Wakili Hilda Dadu amesema Muongozo huo wanao utarajia wanategemea usaidie kuanzia ngazi ya chini ya Kijiji hadi kitaifa ili kutetea haki za binadamu wakiwa wanajiamini kulingana na sheria na taratibu za nchi.

Maadhimisho hayo yameenda sambamba na kumbukizi ya miaka mitano tangu kuanzishwa kwa Mtandao huo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com