Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RC BATILDA AHIMIZA UPIGAJI KURA TANGA UWE ASILIMIA 100

 




Na Mashaka Mgeta ,Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga

MKUU wa Mkoa wa Tanga, Mhe Balozi Dk Batilda Burian, amewahimiza Wakuu wa Wilaya na Wasimamizi wa Uchaguzi mkoani humo, kuhakikisha upigaji kura katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Novemba 27, mwaka huu, unafikia asilimia 100.


Mhe Balozi Dk Batilda ameyasema hayo  Novemba 4, 2024 alipofanya ziara ya kukagua maandalizi ya uchaguzi huo katika halmashauri za wilaya na mji Handeni, akiongozana na Katibu Tawala Mkoa, Pili Mnyema, Kamati ya Usalama (KU) na Kamati ya Uratibu wa Uchaguzi mkoani humo.
Amesema mafanikio yaliyofikiwa kuandikisha asilimia 110.82 ya wapiga kura na kushika nafasi ya pili kitaifa, yamepongezwa na Mhe Rais Dk Samia Suluhu Hassan, hivyo kuibua haja ya kuhakikisha watu wote wanapiga kura.
  
Mkuu wa Mkoa huyo amesema, tofauti na uandikishaji uliofanyika kwa siku 10, upigaji kura utatumia saa 10 katika siku moja, hivyo mikakati ya hamasa, ushawishi na kuwepo mazingira bora yanayowavutia watu wengi kwenda kupiga kura inapaswa kutumika.
‘’Tumefanikiwa kuandikisha wapiga kura kwa asilimia 110.82 kwa zoezi lililofanyika kwa siku 10, sasa tuna saa 10 tu kwa siku moja, kuhakikisha kila aliyejiandikisha anapiga kura ili tuuheshimishe uchaguzi huo na kumheshimisha Mhe Rais Samia Suluhu Hassan,’’ amesema.
Amewakumbusha Wasimamizi wa Uchaguzi kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizopo, ili uchaguzi huo ufanyike na kuthibitika pasipo shaka kuwa ni wa wazi, huru na haki.

Mhe Balozi Dk Batilda amesema, ni dhamira na utashi wa kisiasa wa Mhe Rais Dk Samiakuona uchaguzi huo unatoa fursa pana kwa kila raia, kutumia haki yake ya kikatiba kugombea, ama kumchagua kiongozi anayemtaka.

Amesema pamoja na kufuata sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo, Wasimamizi wa Uchaguzi kwa kushirikiana na Wakuu wa Wilaya wanapaswa kushughulikia na kuondokana na changamoto, ili upigaji kura ufanyike kwa wepesi na haraka.

Ametoa mfano kuwa, mahali penye idadi kubwa ya wapiga kura, viongozi hao wanaweza kufuata taratibu kwa kuongeza idadi ya vituo kabla ya Novemba 7, mwaka huu, lakini kwa kuwashirikisha wadau hususani vyama vya siasa.
Pia amesema mazingira ya siku ya uchaguzi yanaweza kuathiriwa na hali ya hewa, kama vile kuwepo mvua ama jua kali, hivyo upo umuhimu wa kuandaa maturubai ili kukabiliana na hali hiyo.

‘’Tukiyafanya haya na kwa kuzingatia 4R (maridhiano, mabadiliko,ustahimilivu na kujenga upya), tukaufanikisha uchaguzi huu, tutakuwa tumemheshimisha Mhe Rais Samia na kuuheshimisha uchaguzi huu,’’ amesema.

Katibu Tawala Mkoa, Mnyema amesema pamoja na mafanikio yanayoonekana kwenye taarifa za halmashauri hizo, Mhe Mkuu wa Mkoa na timu zake, afanya ziara hizo ili kujiridhisha na uhalisia uliopo, kisha kusaidia utatuzi wa changamoto zinazojitokeza.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Mhe Albert Msando, amesema maandalizi ya uchaguzi huo vikiwemo vifaa vitakavyotumika, yamefikia hatua nzuri, hivyo kuwa na uhakika wa kufanyika kwa uchaguzi huru, wazi na haki.
  
Wakurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya na Mji Handeni, Saitoti Stephen na Mariam Ukwaju, wamemhakikishia Mhe Balozi Dk Batilda kuwa maandalizi yanakwenda vizuri, ikiwa ni pamoja na kuendeleza hamasa na elimu ya mpiga kura kwa wakazi wa maeneo hayo.
Hadi kufikia jana, Mhe Balozi Dk Batilda, ameshazitembelea halmashauri za Lushoto, Bumbuli, Korogwe, Korogwe Mji, Handeni Mji na Handeni.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com