REA KUPELEKA UMEME VISIWA VYOTE TANZANIA BARA

 

*Zaidi ya Visiwa 118 kunufaika na mradi huo

*Zaidi ya Bil. 8/= kutumika

Na REA

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imeanza rasmi safari ya kupeleka umeme katika visiwa vyote Tanzania Bara huku ikiwahakikishia wananchi hao kuwa wote watafikiwa.

Akizungumza wakati wa ziara ya Wabia wa Maendeleo walipotembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na REA, Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi, Meja Jenerali (mstaafu), Jacob Kingu amesema kuwa mradi huo ni dhamira ya serikali kuhakikisha wananchi wote wanapata nishati ya umeme kwa ajili ya kujiletea maendeleo.

Wakati wa ziara hiyo ambayo ilifanyika jana Novemba 6, 2024 katika kisiwa cha Musira kilichopo Wilaya ya Bukoba, mkoani Kagera, viongozi mbalimbali wa Serikali waliambatana na Wabia hao wa Maendeleo ambao Serikali imekuwa ikishirikiana na kuwezesha upatikanaji wa nishati bora vijijini. Wabia hao ni Benki ya Dunia, Serikali ya Norway, Serikali ya Sweden, Umoja wa Ulaya, AFD na ADB.

“Tumekuja kwa ajili ya kufanya vikao vya tathmini ya miradi inayotekelezwa lakini pia hatutafanya vikao tuu, pia tunatemebelea miradi inayotekelezwa pamoja na Wabia wa Maendeleo na hapa Musira tumekuja kuona utekelezaji wa mradi wa mifumo ya umeme jua inayofungwa kwa wananchi.

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Maendeleo ya Umeme kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Styden Rwebangila mesema kuwa serikali imekuwa ikitumia masuluhisho mbalimbali kufikisha umeme kwa wananchi ikiwa ni kwa njia ya kusambaza umeme kawaida au kwa kutoa ruzuku kwenye mifumo ya umeme jua kwa wananchi wanaoishi visiwani ili kuweza kubadilisha maisha yao.

Awali akizungumza kuhusu mradi huo, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Hassan Saidy amesema kuwa mradi huo wenye Zaidi ya gharama ya shilingi Bilioni 8 unatarajiwa kunufaisha wananchi wote waishio katika visiwa kwa kupatiwa mifumo ya umeme jua kwa bei ya ruzuku ambapo serikali inatoa ruzuku ya hadi asilimia 75 ya kufungiwa mifumo hiyo ya umeme jua.

Amesema kuwa zaidi ya mikoa 7 inatarajiwa kunufaika na mradi huo ambapo mifumo Zaidi ya 20,000 inatarajiwa kufungwa visiwa 118 vitapatiwa mifumo hiyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post