●Lengo ni kuweka mazingira bora kuvutia Watalii
Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kutumia fedha na nguvu nyingi katika kuboresha mazingira ya vivutio vya Utalii na Uwekezaji nchini.
Jitihada hizi za Serikali ya awamu ya sita, zimeendelea kwa kuleta mafanikio chanja kwa kasi kubwa, katika Sekta ya Utalii nchini, katika kipindi cha miaka mitatu tangu Rais Samia alipoingia madarakani.
Miongoni mwa jitihada hizo za Serikali katika kuinua Sekta ya Utalii ni kwa kuanzisha miradi katika Hifadhi ya Serengeti Mkoani Mara, ili kuboresha mazingira ya Utalii na Uwekezaji na hatimaye kuinua kipato cha Taifa.
Miradi wa Barabara ya Utalii kilomita 22 uliogharimu takribani Milioni 761.3 na Mradi wa ujenzi wa Vituo Viwili vya kupokea na kukagua wageni (Ikona Gate na Visitors Gate) uliogharimu takribani Shilingi Milioni 143.5 katika Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori Ikona iliyopo Wilaya ya Serengeti Mkoani Mara, ni miongoni mwa Miradi inayotekelezwa na Serikali ya Dkt. Samia.
Mradi hii ya kuendeleza Utalii, imezinduliwa na Dkt. Pindi Chana ambapo ameitaka Jumuiya hiyo kuisimamia na kuitumia vyema miradi hiyo kwa malengo yaliyokusudiwa ya kukuza utalii huku akisisitiza maadili katika utendaji kazi.
Ameipongeza Menejimenti na Jumuiya ya Ikona na kutoa rai kuendelea kushirikiana kwa karibu na Halmashauri za Wilaya, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Wizara ya Maliasili na Utalii katika kutekeleza majukumu yao.
Mhasibu wa Jumuiya ya Ikona, Mariam Magessa amesema, tangu kuanzishwa kwa Jumuiya hiyo, imefanikiwa kupunguza matukio ya ujangili hivyo kupelekea ongezeko la wanyamapori huku ikivutia shughuli za utalii na wawekezaji.
Haya ni matokeo chanya ya uhifadhi yamepelekea kupata jumla ya wawekezaji tisa ambapo nane wamewekeza kwenye utalii wa picha na mmoja kwenye utalii wa uwindaji na kwamba hiyo imekuwa ni sehemu ya mapato ya Jumuiya hiyo.
Hifadhi ya Serengeti ni eneo kubwa la mbuga na misitu katika Tanzania ya kaskazini hasa katika Mikoa ya Mara na Arusha ikipakana na nchi ya Kenya ambapo jina hili la Serengeti limechukuliwa kutoka lugha ya Kimasai hasa, yaani "Serengit" humaanisha "Kiwara kisichoisha", na hifadhi hii ina jumla ya Simba 3,000.