Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAKUTANISHA WADAU KUANDAA MPANGO WA UHIMILIVU NA UENDELEVU WA UKIMWI


Dkt. Jerome Kamwela, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS, akifungua kikao cha Wadau wa Maendeleo na washirika wanaotekeleza afua za mwitikio wa UKIMWI, kilicholenga kujadili Mpango wa Uendelevu wa Kudhibiti UKIMWI nchini. Kikao hicho kinafanyika mkoani Arusha kuanzia tarehe 5 hadi 7 Novemba, 2024.

Na Mwandishi Maalum,Malunde Blog-ARUSHA

SERIKALI kwa Ushirikiano na wadau wa Maendeleo na watekelezaji wa shughuli za Mwitikio dhidi ya UKIMWI wamekutana Mkoani Arusha kwa siku mbili kuandaa Mpango wa uhimilivu na uendelevu wa wa UKIMWI nchini (HIV Response Sustainability Roadmap) kwenye Kikao kinachoratibiwa na Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS).

Mpango huu unalenga kuweka mikakati itakayoiwezesha nchi yetu kuweza kutekeleza afua za UKIMWI kwa fedha za ndani pale ambapo fedha kutoka kwa wafadhili zitapungua zaidi au kukoma kabisa. Mikakati inayowekwa ni ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu baada yamwaka 2030 ambapo inatazamiwa kuwa UKIMWI utakuwa siyo janga la kiafya duniani.

Akizungumza katika kikao hicho Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TACAIDS Dkt. Jerome Kamwela amesema kuwa kupatikana kwa Mpango huo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kuwa na uwezo wa kutekeleza afua za UKIMWI nchini ikiwemo kuziba mwanya wa upungufu wa raslimali za Mwitikio wa UKIMWI nchini, baada kuendelea kupungua kwa raslimali za kutekeleza afua hizo.

“Mpango wa uendelevu wa mwitikio wa UKIMWI ni sehemu ya maandalizi ya kukabiliana na upungufu wa rasilimali za kutekeleza Afua za Mwitikio wa UKIMWI nchini, nawashukuru sana wadau wote mlioshiriki na kufanikisha maandalizi ya Mpango huu, ni matumaini yangu kuwa wote tutashiriki siku ya uzinduzi utakaofika Mkoani Ruvuma tarehe mosi Disemba, 2024 ili tushuhudie kazi tuliyoifanya kwa kipindi chote hiki inazinduliwa tayari kwa matumizi” alisema Dkt Kamwela.

Dkt. Kamwela ameongeza kuwa kazi ya mapambano dhidi ya VVU bado kubwa kwani pamoja na kiwango cha kitaifa cha ushamiri wa maambukizi kupungua, ushamiri katika baadhi ya makundi umeongezeka hasa miongoni mwa makundi ya wachimbaji wadogo wa madini, wavuvi, madereva wa masafa marefu pamoja baadhi ya mikoa nchini.

 Hivyo, ni lazima tuongeze juhudi hadi hapo tutakapoona tunaondoa kabisa maambukizi mapya, watu wote walioambukizwa wanajitambua na kutumia dawa na kuhakikisha kunakuwa hakuna ubaguzi na unyanyapaa kwa WAVIU na wote walioathirika na UKIMWI.

Naye Mkurungenzi Mkaazi wa Shirika la Kimataifa linaloshughulikia UKIMWI (UNAIDS) Dkt. Martin Odiiti akizungumza katika kikao hicho ameshukuru jitihada za Serikali kuona umuhimu wa kutoa kipaumbele katika maamdalizi ya Mpango wa uendelevu wa mwitikio wa UKIMWI nchini.

Dkt. Martin amesema kuwa hii ni nyenzo muhimu sana kwa nchi kwani huu ni mwanzo mzuri wa kuiwezesha nchi kuweza kutekeleza mwitikio wa UKIMWI kwa fedha zake za ndani. Hata hivyo, aliwahakikishia wajumbe wa kikao kuwa kuandaliwa kwa mpango huu hakumaanishi kuwa wafadhili na wadau wa maendeleo wataondoka nchini.

Kikao hicho kilihudhuriwa na wadau kutoka Wizara,wadau wa wamaendeleo na watekelezaji wa Afua za Mwitikio wa UKIMWI.










Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com