Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TAKUKURU YAONGEZA UFANISI KATIKA UKUSANYAJI WA MAPATO KATIKA JIJI LA TANGA

 


Na Oscar Assenga,TANGA


TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Tanga katika kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba 2024 umefanikisha kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato yanayotokana na ada za leseni za biashara.

Hatua hiyo inatokana na ufuatiliaji wa uzingatiaji wa uchukuaji wa leseni za biashara katika sehemu za Biashara mbalimbali katika Halmashauri ya Jiji la Tanga ambapo pia wameongeza ufanisi pia katika ushuru wa nyumba za kulala wageni pamoja na ushuru wa huduma katika Jiji la Tanga.

Hayo yalibainishwa leo na Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Tanga Ramadhani Ndwatah (Pichani )wakati akitoa taarifa ya utendaji kazi wa Takukuru kwa kipindi cha kuanzia Mwezi Julai hadi Septemba mwaka 2024.

Alisema kwamba taasisi hiyo kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Jiji la Tanga walifanya kazi ya kufika kwenye maeneo ya Maduka,Zahanati, Hospitali,Hotel, Vituo vya Mafuta,Bar,Kumbi za Starehe,Shule,Viwandani na Masoko katika kata zote za Halmashauri ya Jiji hilo.

“Tulifanya ufuatiliaji wa ulipaji wa ushuru wa huduma ,ushuru wa nyumba za kulala wageni (Hotel Levy) pamoja na ukaguzi Leseni za Biashara na tulichobaini ni kwamba asilimia 64.35 ya wafanyabiashara hawakuwa na leseni za biashara na zaidi ya asilimia 90 ya wafanyabiashara hawakuwa wamelipa ushuru wa huduma (Service Levy) pamoja na ushuru wa nyumba za kulala wageni (Hotel Levy).

Akizungumzia hatua walizochukua alisema ni kufanya uelimishaji kwa wadau hao juu ya matakwa ya kisheria juu ya ulipaji wa tozo hizo na madhara yake kwao na kwa Halmashauri na Serikali kwa ujumla iwapo tozo hizo hazitalipwa.

Aidha alisema matokeo na mwitikio wa wadau katika utekelezaji wa hatua hizo ni kwamba katika kipindi cha Julai –Septemba mwaka huu Halmashauri ya Jiji la Tanga iliweza kukusanya kiasi cha Bilioni 1,938,185,915.22 sawa na wastani wa asilimia 32.6 ya lengo la mwaka katika vyanzo vya ushuru wa huduma (Service Levy),Ushuru wa Nyumba za Kulala wageni (Hotel Levy).

Alisema pia walikusanya katika ada za leseni za Biashara (Business Licence Free) ukilinganishwa na kiasi cha Sh.Bilioni 1,246,611,579.43 sawa na wastani wa asilimia 22.6 ya lengo la mwaka kilichokusanywa katika kipindi cha April hadi June mwaka 2024 katika vyanzo hivyo.

Hata hivyo alisema katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2024 Takukuru mkoa huo imetekeleza jukumu la uzuiaji wa Rushwa,Elimu kwa Umma na Uchunguzi wa Mashtaka mbalimbali.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com