TANZANIA NA UGANDA ZAKUTANA KUJADILI UIMARISHAJI MPAKA WA KIMATAIFA

Katibu Tawala mkoa wa Kagera Bw, Stephen Ndaki (katikati), Naibu Balozi wa Uganda nchini Tanzania Balozi Elizabeth Allimadi (wa kwanza kulia), Mwakilishi wa Balozi wa Tanzania nchini Uganda Bw. Toritoi Bunto (wa kwanza kushoto) Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw. Hamdouny Mansoor (wa pili kushoto) na Mkuu wa ujumbe wa Uganda Bi. Jacquiline Banana Wabyona (wa pili kulia) wakiwa katika picha mara baada ya ufunguzi wa kikao cha kamati ya pamoja ya Uimarishaji mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Uganda tarehe 5 Novemba 2024.

**********************

Na Munir Shemweta, WANMM Bukoba

Kikao cha Kamati ya Pamoja cha Wataalamu wa Tanzania na Uganda (JTC) kimeanza mkoani Kagera nchini Tanzania kujadili uimarishaji mpaka wa kimataifa baina ya nchi hizo.

Kikao hicho kimeanza tarehe 5 Novemba 2024 na kutarajiwa kumalizika Novemba 7, 2024 kinafanyika katika manispaa ya Bukoba mkoani Kagera na kuhusisha wataalamu kutoka nchi za Tanzania na Uganda.

Akifungua kikao hicho cha siku tatu kwa niaba ya Mkuu wa mkoa wa Kagera Hajat Fatma Abuubakar Mwasa, katibu Tawala mkoa wa Kagera Bw. Stephen Ndaki amesema, Tanzania imejipanga kikamilifu kutekeleza zoezi la uimarishaji mpaka wa kimataifa kwa ajili ya ustawi wa nchi hizo mbili.

Amebainisha kuwa, uimarishaji mpaka wa kimataifa kati ya Tanzania na Uganda una lengo la kuweka usimamizi mzuri wa mpaka baina ya nchi hizo pamoja na kukuza amani, upendo, usalama na maisha ya watu wake.

Kupitia hotuba hiyo ya Mkuu wa mkoa wa Kagera, Bw. Ndaki amesema, Tanzania na Uganda zimekuwa na mahusiano mazuri ikiwemo tamaduni zinazofanana alizozieleza kuwa, zimewezesha wananchi wa nchi hizo mbili kuishi kwa upendo.

"Ni imani yangu kila mshiriki katika kikao hiki atatumia muda kuhakikisha uimarishaji mpaka wa kimataifa baina ya nchi zetu unakuwa na matokeo mazuri kwa ustawi wa nchi na wananchi wetu" amesema.

Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye ni mkuu wa timu ya Tanzania katika kikao hicho Bw. Hamdouny Mansoor amesema, mkutano huo ni utekelezaji wa mpango wa Umoja wa Afrika kuhusu uimarishaji wa mipaka ya kimataifa kwa nchi za Afrika kufikia mwaka 2027.

"Ni nia ya Umoja wa Afrika kuzifanya nchi za Afrika kuwa na amani pasipo migongano wakati wa zoezi zima za uimarishaji mipaka ya kimataifa" amesema Mansoor.

Kwa upande wake Mkuu wa ujumbe wa timu ya wataalamu kutoka Uganda Bi. Jacqueline Banana Wabyona ameihakikishia Tanzania ushiriki mzuri kwenye kikao hicho kwa lengo la kufikia matokeo chanya ya uimarishaji mpaka kati ya Tanzania na Uganda.

Mpaka wa Tanzania na Uganda una urefu wa takriban km 397.8 ambapo kati ya hizo km109 ni nchi kavu , km 42.8 ni sehemu ya mto kagera na km 246 ni sehemu ya ziwa victoria.

Zoezi la uimarishaji mipaka ya kimataifa ni utekelezaji wa makubaliano ya Umoja wa Afrika kuwa, ifikapo mwaka 2027 mipaka baina ya nchi za Afrika iwe imeimarishwa.

Tanzania imepakana na nchi 10 ambazo ni Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, DRC, Zambia, Malawi, Msumbiji, Comoro na Shelisheli huku mipaka baina ya nchi hizo ikiwa imegawanyika katika sehemu mbili za nchi kavu na majini.
Kamati ya pamoja ya wataalamu kutoka Tanzania na Uganda wakiwa katika kikao cha Uimarishaji Mpaka wa Tanzania na Uganda mkoani Kagera tarehe 5 Novemba 2024.
Wajumbe wa Tanzania katika kikao cha kamati ya pamoja kati ya Tanzania na Uganda kuhusu uimarishaji mpaka wa kimataifa wan chi hizo mbili tarehe 5 Novemba 2024 mkoani Kagera.
Wajumbe wa Uganda katika kikao cha kamati ya pamoja kati ya Tanzania na Uganda kuhusu uimarishaji mpaka wa kimataifa wa nchi hizo mbili tarehe 5 Novemba 2024 mkoani Kagera.
Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Upimaji na Ramani Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bw.Joseph Ikorongo akiwasilisha taarifa ya Tanzania wakati wa kikao cha pamoja kati ya Tanzania na Uganda kuhusu uimarishaji mpaka wan chi hizo tarehe 5 Novemba 2024 mkoani Kagera.
Kamati ya pamoja ya wataalamu kutoka Tanzania na Uganda wakiwa katika kikao cha Uimarishaji Mpaka wa Tanzania na Uganda mkoani Kagera tarehe 5 Novemba 2024.
Katibu Tawala mkoa wa Kagera Bw. Stephen Ndaki (katikati waliokaa) pamoja na viongozi wengine wakiwa katika picha ya pamoja na wajumbe wa kamati ya pamoja ya wataalamu wa Tanzania na Uganda wakati wa kikao cha uimarishaji mpaka wa Tanzania na Uganda tarehe 5 Novemba 2024.
Katibu Tawala mkoa wa Kagera Bw. Stephen Ndaki (kulia) akifungua mkutano wa kamati ya pamoja ya wataalamu wataalamu wa Tanzania na Uganda wakati wa kikao cha uimarishaji mpaka wa Tanzania na Uganda tarehe 5 Novemba 2024. (PICHA NA WIZARA YA ARDHI)

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post