Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdouny Mansour (wa pili kushoto) na Bi Jacqueline Banana Wabyona ambaye ni Mkuu wa ujumbe wa Uganda (wa pili kulia) wakisaini hati ya makubaliano ya uimarishaji mpaka wa Tanzania na Uganda katika kikao kilichofanyika jana mkoani Kagera.
********************
Na Munir Shemweta, WANMM Bukoba
Tanzania na Uganda zimetia saini makubaliano ya uimarishaji mpaka wa kimataifa baina ya nchi hizo mbili.
Makubaliano hayo yalifikiwa wakati wa mwisho wa kikao cha Kamati ya Pamoja ya Wataalamu (JTC) kati ya nchi hizo kilichokuwa na lengo la kujadiliana namna ya kuimarisha mpaka wa Tanzania na Uganda.
Utiaji saini makubaliano hayo ulifanyika jana katika manispaa ya Bukoba mkoani Kagera kati ya Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdouny Mansour na Bi Jacqueline Banana Wabyona ambaye ni Mkuu wa ujumbe wa wataalamu kutoka nchini Uganda.
Wakati wa utiaji saini makubaliano hayo, viongozi wote wawili walionesha kuridhishwa na namna wataalamu wa nchi hizo mbili walivyoshiriki majadiliano ya pande hizo mbili na hatimaye kufanikisha kusainiwa kwa makubaliano kati ya Tanzania na Uganda.
Kikao cha Kamati ya pamoja cha wataalamu wa Tanzania na Uganda (JTC) kilianza tarehe 5 Novemba 2024 mkoani Kagera ambapo kimejadili mambo mbalimbali ha uiamarishaji mpaka wa kimataifa baina ya nchi hizo.
Mpaka wa Tanzania na Uganda una urefu wa takriban km 397.8 ambapo kati ya hizo km109 ni nchi kavu , km 42.8 ni sehemu ya mto kagera na km 246 ni sehemu ya ziwa victoria.
Zoezi la uimarishaji mipaka ya kimataifa ni utekelezaji wa makubaliano ya Umoja wa Afrika kuwa, ifikapo mwaka 2027 mipaka baina ya nchi za Afrika iwe imeimarishwa.
Bw. Hamdouny Mansour, Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdouny Mansour (kushoto) na Bi Jacqueline Banana Wabyona, Mkuu wa ujumbe wa wataalamu kutoka nchini Uganda (kulia) wakibadilishana hati za makubaliano mara baada ya kutia saini makubaliano ya uimarishaji mpaka wa Tanzania na Uganda baada ya kikao cha pamoja kilichofanyika jana mkoani Kagera.
Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdouny Mansour (kushoto) na Bi Jacqueline Banana Wabyona ambaye ni Mkuu wa ujumbe wa wataalamu kutoka nchini Uganda (kulia) wakionesha hati za makubaliano mara baada ya kutia saini makubaliano ya uimarishaji mpaka wa Tanzania na Uganda katika kikao cha pamoja kilichofanyika jana mkoani Kagera.
Mkurugenzi wa Upimaji na Ramani wa Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Hamdouny Mansour (wa pili kushoto) na Bi Jacqueline Banana Wabyona, Mkuu wa ujumbe wa Uganda (wa pili kulia) wakipongezana mara baada ya kubadilishana hati za makubaliano ya uimarishaji mpaka wa Tanzania na Uganda wakati wa kikao cha pamoja kilichofanyika mkoani Kagera. Kulia ni Naibu Balozi wa Uganda nchini Tanzania Balozi Elizabeth Allimadi na kushoto ni Mwakilishi wa Balozi wa Tanzania nchini Uganda Bw. Teritoi Bunto (PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
Social Plugin