TBS YAKUTANA NA WAINGIZAJI WA BIDHAA ZA VYAKULA NCHINI


Na Mwandishi Wetu

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limesema bidhaa nyingi za vyakula vinavyofungashwa  na visivyokidhi vigezo vya usalama na ubora ,vimekuwa vikikataliwa kusajiliwa na kutoruhusiwa kuingizwa nchini.

Kwa uzuiaji wa bidhaa hizo,TBS imeweza kuchangia kwa kiasi kikubwa kulinda na kuendeleza afya  ya jamii na soko la Tanzania dhidi ya bidhaa za chakula zisizo na usalama na ubora.

Hayo yamesemwa leo Novemba 6,2024 jijini Dar es Salaam na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, David Ndibalema, wakati wa Mkutano wa TBS na waingizaji wa vyakula nchini uliofanyika jijini Dar es Salaam jana.

Dibalema alisema tangu TBS ipewe jukumu la kusimamia sheria ya usalama wa chakula nchini, kwa kutumia dirisha la usajili katika kumlinda na kuendeleza afya ya mlaji imeweza kupiga hatua mbalimbali ambazo zimeweza kuzuia bidhaa za  chakula zisizo na usalama na ubora kutoingia nchini wala kusambaa sokoni.

Alisema ikumbushe kuwa usajili wa bidhaa za vyakula vilivyofungashwa ni takwa  la kisheria linalolenga kuhakikisha kuwa vyakula salama na bora ndivyo vinaruhusiwa kuingizwa sokoni ili kulinda na kuendeleza afya ya mlaji na jamii kwa ujumla.

Alisema usajili huo pia unasaidia kulinda na kuendeleza biashara  kwa mujibu wa makubaliano ya kimataifa na sera za nchi  za kiuchumi zilizopo hasa zile zinazohusu uwezeshaji wa uwepo  wa mazingira mazuri ya ufanyaji biashara nchini.

"Nimefurahi sana kushiriki mkutano huu wa wafanyabiashara wanaoagiza na kuingiza bidhaa za chakula kilichofunganishwa nchini,muitikio wenu ni ishara kuwa mkutano  huo una umuhimu mkubwa katika kuhakikisha kuwa bidhaa zinazotengenezwa na viwanda husika ,kisha kuingizwa nchini usalama na ubora wake  unafahamika kwa kutumia vigezo vya kisayansi  bila kukwamisha ufanyaji biashara.

"Lengo kuu likiwa ni kulinda na kuendeleza afya ya mlaji pamoja na kulinda soko la Tanzania dhidi ya bidhaa za vyakula visivyo salama na bora,"alisema Ndibalema.

Alisema mkutano huo utatoa fursa kupata uelewa wa pamoja ili shughuli za kusimamia salama wa chakula nchini ziweze kuwa ni zenye ufanisi kupitia nguvu ya pamoja baina ya wafanyabiashara, walaji na wasimamizi.

Aidha Ndibalema  alisema matarajio ya shirika lao kupitia mkutano huo utasaidia kuongeza ufahamu wa mambo mbalimbali  kutoka kila upande ikiwemo mwingizaji bidhaa kufahamu sababu zianzopelekea wakati mwingine bidhaa yake anayotaka.kuingiza nchini.kukataliwa usajili na kujua tathimini zinazofanyika kwa bidhaa kukataliwa kusajiliwa.

Awali akimkaribisha mgeni Ndibalema, rasmi, Meneja wa Usajili wa Bidhaa na Majengo wa TBS, Habakuki Kalebo,  alisema wamekuwa wakipokea maoni na maombi mbalimbali kutoka kwa wadau wa Shirika yanayohusu namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali katika utendaji wao na kuboresha huduma zao kwa jamii wanayoihudumia.

"Mkutano huu unatarajia kuchangia kwa kiasi kikubwa kuwa na uelewa wa pamoja baina ya pande mbili hususan kwa baadhi ya maeneo ambayo wamebaini kuwa wanauelewa mdogo au tofauti baina ya pande hizo mbili,"alisema Kalebo.

Alisema moja ya mbinu ambayo itachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma kwa wateja na wakati huo kuongeza ufanisi wa majukumu waliyopewa kisheria ni kuwa na mkutano rasmi wa mara kwa mara na wadau wao wakiwemo wafanyabiashara wanaoingiza nchini bidhaa zinazosajiliwa na TBS.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post