Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TGNP YAWAJENGEA UWEZO VIONGOZI WAJAO WA KIKE KUPITIA MAFUNZO YA UONGOZI VYUO VIKUU


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP), kupitia jukwaa la Young Feminist Forum, wameendesha mafunzo kwa wanafunzi wa kike kutoka vyuo vikuu 13 nchini yenye lengo la kuwajengea uwezo wa kuwa viongozi, kuanzia katika ngazi ya chuo hadi watakaporudi mtaani.

Mafunzo haya ni muhimu kwa kuwa yanalenga kuongeza uongozi wa wanawake katika nyanja mbalimbali si tu za kisiasa bali pia kijamii na kiuchumi.

Akizungumza leo Novemba 28,2024 wakati akifungua mafunzo hayo, Kaimu Mkuu wa Idara ya Ujenzi wa nguvu za pamoja, Flora Ndaba amesema kupitia jukwaa lao wanahitaji kutengeneza viongozi ambao watabeba ajenda za wanawake wanapokuwa katika nafasi za uongozi na sio kwa ajili ya maslahi yao binafsi.

"Siyo tu awe kwenye hiyo nafasi kwa sababu moja ya kimaslahi,lakini kusemea Mambo Yale ambayo hayasemwi yanayowakabili kama wanawake"Flora ameeleza.

Kwa upande wake, Afisa Taasisi ya Doyenne, Barbara Mlata amesema kwenye mafunzo hayo watajadili changamoto wanazopitia wanafunzi viongozi na kuwajengea uwezo ili wanaporudi vyuoni waweze kushiriki kikamilifu katika masula ya uongozi.

Sambamba na hayo amesema kupitia mafunzo hayo watawashauri na kuwahamasa Vijana hao kushiriki katika masuala ya uongozi ili kuongeza nafasi za wanawake viongozi nchini pamoja na vyuoni.

Nae, Mwenyekiti wa Jinsia Chuo Cha Taifa Cha Usafirishaji (NIT) Leticia Samson amesema wanatarajia mafunzo hayo kuleta matokeo chanya kwa kuwapatia uthubutu wasichana wanaonolewa mahali hapo kwani watoto wa kike wanaweza kuongoza sawa na watu wa jinsia nyingine.

Vilevile,Kiongozi chuo Cha Utumishi wa Umma, Radhia Omary ameeleza kuwa mafunzo hayo yatawajengea uwezo wa kukabiliana na changamoto za uongozi kuanzia anapokua chuoni hata pia atakapo hitimu chuo anaporudi katika jamii atatumia ujuzi huo kukemea vitendo vya ukatili.

Sambamba na hayo Mwanafunzi wa Chuo Kikuu Cha Kampala Jijini Dar es Salaam (KIUT),Veronica Charles amesema mafunzo hayo yanawajengea kujitambua ambapo sio tu katika uongozi wa kundi au jamii lakini pia katika uongozi kwenye nyanja ya kiuchumi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com