Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TOTALERNEGIES MARKETING TANZANIA LTD KUPITIA MFUKO WA ELIMU WA TAIFA YATOA KATONI 360 ZA TAULO ZA KIKE KWA SHULE NNE ZA SEKONDARI.

Kaimu Mkurugenzi Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi Bw. Masozi Nyirenda akiongea katika hafla ya kukabidhi katoni 360 za taulo za kike zilizotolewa na TotalEnergies Marketing Tanzania.


**********************

Dodoma

Kampuni ya TotalEnergies Marketing Tanzania Ltd leo tarehe 22 Novemba 2024 imekabidhi katoni 360 za taulo za kike zenye thamani ya takribani Sh. Milioni 25.5 ikiwa ni sehemu ya kuchangia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia kwa lengo la kuwasaidia watoto wa kike kuendelea kufurahia masomo hata wanapokuwa katika siku za hedhi.

Kukabidhiwa kwa taulo hizo za kike katoni 360 hii leo kunaifanya kampuni hiyo ndani ya mwaka 2024 kuwa imetoa jumla ya katoni 500 zenye thamani ya Sh milioni 35.4 ambazo zimesambazwa katika shule saba zikijumuisha za msingi na sekondari.

Hafla fupi ya kukabidhi taulo hizo za kike imefanyika Makao Makuu ya TEA yaliyoko Ilazo Extension Jijini Dodoma ambapo pia imehudhuriwa na wawakilishi wa shule nne za sekondari zitakazonufaika ambazo ni; Lemira iliyoko Hai Kilimanjaro, Sitalike ya Mkoani Katavi, Manunus Mkombozi ya Same Kilimanjaro na Isack Kamwelwe ya Mkoani Katavi.

Shule nyingine zilizonufaika na taulo hizi za kike ni pamoja na Shule ya Sekondari Songwe ya Mkoani Songwe, Kilombero na Njiwa zote za Mkoani Morogoro pamoja na Sisters of Mary iliyoko Kisarawe Mkoani Pwani.

Kwa upande wa TEA hafla hiyo imeongozwa na Kaimu Mkurugenzi Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi Bw. Masozi Nyirenda ambapo upande wa TotalEnergies Marketing Tanzania Ltd imewakilishwa na Mkurugenzi wa Sheria na Mahusiano ya Kampuni, Bi Getrude Mpangile.

Mbali na kuchangia taulo za kike, Kampuni ya TotalErnegies Marketing Tanzania Ltd mwaka huu imetoa msaada wa madawati 200 katika shule tatu katika mikoa ya Pwani na Dar es Salaam yakiwa na thamani ya Sh. milioni 25. 9 kutokana na kuingia makubaliano ya kushirikiana na TEA katika kutoa misaada ya kuboresha mazingira ya kujifunza na kufundishia nchini.

Mamlaka ya Elimu Tanzania inalo jukumu la kuhamasisha wadau mbalimbali wa Elimu ikiwemo mashirika ya umma, mashirika binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali, asasi mbalimbali na watu binafsi kuchangia maendeleo ya elimu kwa kuchangia rasilimali fedha katika Mfuko wa Elimu wa Taifa. Mchangiaji katika Mfuko wa Elimu ananufaika kwa njia zifuatazo;
Kupata Hati ya Utambuzi wa Uchangiaji wa Elimu (Certificate of Educational Appreciation) kwa mujibu wa Kifungu cha 12 cha Sheria ya Mfuko wa Elimu ya mwaka 2001.
Kupata nafuu ya kodi kutoka kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa mujibu wa Kifungu cha 16 (1) cha Sheria ya Kodi ya Mapato Sura 332 marejeo ya mwaka 2019.
Kutangazwa na kutambuliwa kitaifa, ambapo mchangiaji huandikwa katika rejesta ya kudumu ya wachangiaji wa elimu.

Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ni Taasisi ya Umma inayofanya kazi chini ya usimamizi wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia. TEA inaratibu Mfuko wa Elimu wa Taifa ambao unasaidia jitihada za Serikali katika kuboresha miundombinu ya elimu kwa lengo la kuongeza ubora wa elimu na upatikanaji wake kwa usawa.

Mkurugenzi wa Sheria na Mahusiano ya Kampuni wa TotalEnergies Marketing Tanzania Ltd Bi Getrude Mpangile akielezea dhamira yao ya kuchangia kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika hafla ya kukabidhi katoni 360 za taulo za kike.
Kaimu Mkurugenzi Utafutaji Rasilimali na Usimamizi wa Miradi Bw. Masozi Nyirenda (kulia) akipokea taulo za kike kutoka kwa Mkurugenzi wa Sheria na Mahusiano ya Kampuni wa TotalEnergies Marketing Tanzania Ltd Bi Getrude Mpangile tayari kwa ajili ya kuzipatia shule nne zitakazonufaika.
Walimu kutoka shule nne ambazo ni wanufaika wa taulo za kike wakikabidhiwa taulo hizo kwa ajili ya kuwapelekea wanafunzi wa kike kwenye shule zao.
Baadhi ya watumishi wa Mamlaka ya Elimu Tanzania, TotalEnergies Marketing Tanzania na walimu kutoka shule nne nufaika wakiwa katika picha ya Pamoja mara baada ya hafla ya kukabidhiwa jumla ya katoni 360 za taulo za kike kwa lengo la kuwasaidia wanafunzi wa kike kusoma katika hali ya usafi muda wote.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com