Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

USHAMIRI WA VVU WAONGEZEKA KWA MADEREVA WA MASAFA MAREFU, WACHIMBAJI WADOGO WA MADINI NA WAVUVI




Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Ummy Nderiananga(Katikati) akizungumza na Waandishi wa habari(hawapo pichani)kuhusu maadhimisho ya siku ya ukimwi Duniani leo November 14,2024 Jijini Dodoma

Na Dotto Kwilasa,Dodoma

KUELEKEA maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani, idadi ya watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi nchini inakadiriwa kuwa 1,540,000 kwa mwaka 2022/23 ukilinganisha na takribani watu 1,700,000 mwaka 2016/17

Hayo yameelezwa leo November 14,2024 Jijini hapa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge na Uratibu Ummy Nderiananga wakati akizungumza na Waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani kwa mwaka 2024.

Amesema ushamiri wa Virusi vya UKIMWI (VVU) Kitaifa ni asilimia 4.4 ikilinganishwa na asilimia 4.7 kwa mwaka 2026/17.

Nderiananga ameeleza kuwa licha ya mafanikio hayo bado kumekuwa na kuongezeka kwa ushamiri miongoni mwa baadhi ya makundi yakiwemo vijana kati ya miaka 15-24, madereva wa masafa marefu, wachimbaji wadogo wa madini na wavuvi.

"Kwa niaba ya Serikali napenda kuchukua fursa hii kuendelea kuwasihi wananchi wote kujikinga na kutumia dawa kwa usahihi kwa wale walio jitambua wanaishi na maambukizi,jamii pia shirikianeni na wadau wote kupanga na kutekeleza shughuli za kudhibiti VVU kwa kuzingatia vipaumbele na mahali walipo, " amesema
Mbali na hayo ametaja maeneo ya vipaumbele kuwa ni pamoja na kuimarisha afua za VVU na UKIMWI kwa vijana kwani takwimu zinaonesha kuwa kundi la vijana wa umri wa miaka 15 hadi 24 linachangia maambukizi mapya ya VVU kwa kiwango kikubwa zaidi na kuliweka kundi hilo kuwa kwenye hatari kubwa zaidi ya kupata maambukizi hayo.

Akizungumzia maadhimisho hayo ambayo huratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Tume ya kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Naibu Waziri huyo ameeleza kuwa yanalenga kutathmini mwelekeo wa kudhibiti VVU na UKIMWI nchini ikiwa ni pamoja na kuhamasisha jamii kuendelea kushiriki kwenye ajenda ya kudhibiti maginjwa hayo.

"Malengo mengine ni kutafakari changamoto, mafanikio na uimarishaji wa mikakati mbalimbali ya kudhibiti UKIMWI na kuhamasisha utekelezaji wa kaulimbiu inayotolewa kila mwaka kulingana na vipaumbele vya kidunia na kwa kuzingatia muktadha wa kitaifa, " amefafanua

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa TACAIDS Dkt Jerome Kamwela ameeleza kuwa kwa mwaka huu maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yatafanyika kitaifa Mkoani Ruvuma kwa kaulimbiu ya kulinda afya ya watu wote kwa kuchagua njia sahihi ili kutokomeza UKIMWI.

Dkt. Kamwela amesema wadau wote chini ya Uratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu wanaendelea na maandalizi ya maadhimisho hayo ikiwemo utoaji wa taarifa mbalimbali za udhibiti wa VVU na UKIMWI kwa njia tofati na kwamba kwenye maadhimisho hayo kutakuwa na huduma za upimaji wa hiari wa VVU kwa wiki nzima kuanzia tarehe 24 November hadi December 1,mwaka huu.
"Huduma hizi zitatolewa kwenye mabanda ya maonesho yakayokuwa kwenye uwanja wa michezo wa Majimaji Mkoani Ruvuma,pamoja na yote hayo ndani ya wiki moja kabla ya kilele kutakuwa na matukio mbalimbali ikiwemo la November 22,2024 ambalo wadau watagawana mabanda ya maonesho, nawahimiza wadau wote kuwahi ili wapate muda wa kuandaa shughuli zao na kuwa tayari kwa ajili ya maonesho na utoaji huduma, "amesema

Pamoja na hayo ametumia nafasi hiyo kuishauri jamii kuendelea kulinda afya na kueleza kuwa UKIMWI sio adhabu ya kifo kwa sababu mtu mwenye virus hivyo akijitambua mapema anaweza kuishi maisha marefu .

" Virus vya UKIMWI vipo, kila mtu achukulie fursa kupima na kuanza dawa mapema na kuepuka maambukizi mapya,lazima tujifunze kuwakinga na wengine ili kuishi maisha marefu na kufanya uzalishaji wa uchumi kwa Uhuru wa kutokuwa na hofu ya magonjwa,"amesisitiza Dkt. Kamwela















Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com