Na Dotto Kwilasa,Dodoma
SERIKALI kupitia Wizara ya fedha imewataka wafanyabiashara kote nchini kukopa mikopo rasmi kwenye taasisi za kifedha zinazotambulika ambazo zitaleta unafuu wa riba na kuwa na faida kwenye uchumi wa mtu mmoja mmoja.
Hayo yameelezwa leo November 4,2024 Jijini Dodoma na Waziri wa Fedha Dk. Mwigulu Nchemba kwenye Uzinduzi wa utoaji wa hati fungani ya Bondi Yangu inayoendeshwa na Benki ya Azania yenye lengo la kupanua huduma za kifedha ili kunufaisha makundi ya kijamii ikiwemo vijana na wanawake ambayo inayotarajia kukusanya jumla ya shilingi bilioni 100 kupitia soko la mitaji.
Amesema wafanyabiashara wengi wanashindwa kutimiza malengo yao kutokana na mitaji yao kuwa na riba kubwa na kueleza kuwa uzinduzi huo ni kielelezo tosha cha umuhimu wa ukuaji wa Sekta ya Fedha hali itakayoongeza umakini kwenye jamii kuhusu namna ya kutumia huduma za kifedha zinazotambuliwa na Serikali.
"Serikali ina imani kubwa na sekta binafsi katika kuchangia maendeleo ya nchi yetu,Sekta hii ikiwemo huduma za Benki imeendelea kufanya vizuri na kuwa na mchango mkubwa katika kuchagiza kukua kwa uchumi na kuleta maendeleo kwa Watanzania," amesema na kuongeza;
Kwa kutambua mchango mkubwa wa Sekta ya Fedha katika maendeleo na kukua kwa uchumi wetu Serikali imekuwa ikiweka juhudi katika kuhakikisha kunakuwa na mazingira mazuri ya kisera na kisheria katika kuwezesha ustawi wa Sekta ya Fedha katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na benki, bima, masoko ya mitaji na dhamana, mifuko ya uwezeshaji na mengineyo, "amesisitiza Dk. Mwigulu.
Amesema kwa upande wa Benki, huduma zimeendelea kuongezeka nchini kama inavyojidhihirisha kwa kuwapo kwa huduma na bidhaa mbalimbali za benki na kwamba ubora huo unapunguza kiwango cha mikopo chechefu.
"Serikali chini ya uongozi wa Rais wetu wa awamu ya sita Dkt. Samia Suluhu Hassan iliandaa kwa kushirikiana na wadau mbalimbali Mkakati wa Kugharamia Miradi ya Maendeleo kwa njia Mbadala (APF) ikiwa ni utekelezaji wa Mpango Mkuu wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa Mwaka 2020/21-2029/30 ambapo miongoni mwa malengo yake ni kuhakikisha Taasisi mbalimbali zinatumia vyanzo bunifu na mbadala ambavyo vipo na vina uwezo wa kutoa mitaji, "ameeleza
Akizungumzia Mkakati huo amesema ulizinduliwa rasmi Mei 2021 na kuvitaja vyanzo hivyo mbadala kuwa ni pamoja na hatifungani za aina mbalimbali ikiwa pamoja na za kijani, bluu na nyingine za aina hiyo, matumizi ya mitaji halaiki (crowdfunding), kutafuta mitaji kupitia masoko ya hisa (equity financing), PPP, Hatifungani za Miundombinu (Infrastructure Bond), Hatifungani za Mamlaka za Serikali za Mitaa (Municipal Bonds); Lease Financing; Diaspora Bonds; na nyinginezo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Dk. Esther Mang'enya ametaja viwango vya riba vya Hati Fungani hiyo kuwa ni rafiki kwa mtanzania hata yule mwenye kipato cha chini kuweza kumudu, Shilingi 500,000 tu kwa riba ya asilimia 12.5 kwa mwaka, na kutoa gawio la faida kila baada ya miezi mitatu.
"Hii ni tofauti na hatifungani nyingi zinazotoa gawio la faida kila miezi sita (6),pia hata ukomo wa miaka minne (4) ni muda rafiki wa uwekezaji" amesema
Pamoja na mambo mengine amesema, 2023 ulikuwa ni mwaka wa kwanza wa utekelezaji wa mpango mkakati wa Benki hiyo na kwamba ilifanikiwa kupata matokeo mazuri na kukuza mizania.
Dk. Mang'enya amefafanua kuwa mizania hiyo ilifikia Trilioni 2.3 na kutengeneza faida ya Bilioni 29 na kufanikiwa kutoa gawio la shilingi Bilioni 8.9
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Azania CPA Felix Maagi ameeleza kuwa uzinduzi wa hati hiyo fungani utaongeza chachu ya maendeleo kwa Taifa na kuiunga mkono serikali kwa kutoa mchango katika kufanikisha mipango mbalimbali ya kimkakati na hasa ushirikishwaji wa kifedha kwa vikundi vya kinamama na vijana kupitia fedha zitakazopatikana kwa mauzo ya hati fungani hii.
" Benki ya Azania imekuwa mstari wa mbele katika kutoa huduma mbalimbali za kibenki kwa vikundi mbalimbali na mradi huu ni katika kuimarisha utoaji wa huduma zenu kwa makundi yaliyo nje ya wigo wa kibenki, makusanyo ya hati fungani hii yataleta chachu kubwa katika kuwawezesha wale ambao wanakwama kupata huduma rasmi za kibenki kuwezeshwa kiuchumi, "amesisitiza Maagi
Amesema Katika kukuza uchumi wa Watanzania, benki hiyo imeazisha akaunti maalum kwa ajili ya kuwawezesha wafanyabiashara na kwamba hatua hiyo inachochea uzalendo.
Social Plugin