Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VITUO 5405 VITATUMIKA KUPIGIA KURA UCHAGUZI MKOA WA TANGA



Na Hadija Bagasha - Tanga

MKUU wa Mkoa wa Tanga Balozi, Dkt. Batilda Burian amesema kwamba katika mkoa wa Tanga kuna vituo 5405 vitakavyotumika kupigia kura katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika novemba 27  huku akieleza vifaa vyote vimekwisha kwenda kwenye maeneo yote.

Dkt Burian aliyasema hayo leo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea uchaguzi huo ambap alisema kwamba na maeneo yote ambayo yatatumika kwenye upigaji wa kura wameshayakagua na utayari upo.

Alisema kwamba anaamini watu wa Tanga ni waastaarabu na wasiotaka fujo waende kupiga kura wakijua kwamba Tanga ni ya amani na Tanzania ni ya amani.

“Twendeni tukapige kura kwa sababu muda wa kupiga kura ni mchache kuliko tuliotumia kwenye uandikishaji na vituo vya kupiga kura vitafunguliwa asubuhi na kufungwa saa kumi na mbili jioni ingawa saa 10 ndio muda wa mwisho kufika kituoni hivyo nawasihi wananchi tutumie fursa ya kupiga kura ili tuweze kuchangua viongozi”, amesema Mkuu huyo wa Mkoa.

 Aidha ametoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye uchaguzi huo kama walivyofanya wakati wa zoezi la uandikishaji ili kupata watu wengi kupiga kura na kuweza kufikia malengo ambayo wanayategemea kama mkoa wanataka zoezi liwe kubwa watu wote waweze kushiriki.

“Lakini Katika mchakato mzima wa rufaa zilizokuwepo ni 298 katika hizo zilizorejeshwa ni 264 na rufaa 34 zilizoshindwa kurejeshwa kutokana na kukosekana vigezo vya kikanuni vya kuruhusu rufaa hizo ziweze kupitishwa hizo”,amesema.

Aidha alisema rufaa 264 ambazo zimepitishwa nyengine ni katika kusaidia watu wote washiriki kwenye uchaguzi huo huku akieleza mambo ya hitilafu mbalimbali za makosa ya kiuandishi mengi yalivumiliwa ili kuweza kuona wanakuwa na demokrasia nzuri na vyama vyote vinashiriki kwene uchagzu huo.

Hata hivyo alivitaja vyama ambavyo vitashiriki kwenye uchaguzi huo kuwa ni CCM,ACT Wazalendo,CUF,Chadema,NCCR ,NLD,SAUTI na hao ndio wengi wamesimamisha wagombea pamoja na uwepo wa vyama nyengine kama UDP na vyengine zinazojukiana nchini.

“Katika Mkoa wetu huu tuna Vijiji 763, vitongoji 4528, mitaa 270 na katika Halmashauri 11 miji midogo mitatu Mombo, Lushoto na Muheza lakini pia tuna Jumla ya Kata 245 na katika kipindi cha uandikishaji, hatua ya mchujo na kwenda kwenye kampeni hatujapata changamoto yoyote ile sio kwenye vyama vya siasa hiyo yote ni kuhakikisha tunakwenda kwenye uchaguzi tukiwa wamoja na kusonga mbele”, amesema.

Hata hivyo Mkuu huyo wa Mkoa aliwashukuru wananchi wote waliojitokeza kwenye zoezi la uandikishaji ambapo Tanga iliibuka kidede namba mbili  kwenye zoezi la uandikishaji .

“Tuliweza kuvuka lengo la uandikishaji tulitegemea kuandikisha  watu Milioni 1.4 lakini tumekwenda kuandikisha watu milioni 1.6 na kupelekea Mkoa kuwa asilimia 110.6 nawapongeza wananchi ,wanahabari kwa jinsi mlivyopeleka hamasa na hamasa kubwa wananchi”,amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com