Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WABIA WA MAENDELEO WAAHIDI KUENDELEA KUSHIRKIANA NA SERIKALI KUTEKELEZA MIRADI YA REA

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mhe. Fatma Mwassa ameupongeza Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa kazi kubwa ya kufikisha umeme vijijini ambapo imekuwa ni chachu katika kuboresha huduma za kijamii vijijini pamoja na uchumi wa wananchi.

Mhe. Mwassa ametoa pongezi hizo leo Novemba 8, 2024 Mkoani Kagera wakati akifungua Mkutano wa Pili wa Mwaka kati ya Wabia wa Maendeleo katika Sekta ya Nishati (EDPG) pamoja na REA uliolenga kufanya tathmini ya miradi iliyotekelezwa na wakala huo katika kipindi cha mwaka mmoja.

“Wakati REA inaanzishwa watu wengi walifikiri ni ndoto ya juu sana. Lakini kwa matokeo ya sasa kila kijiji kina umeme na si ndoto tena. Ni mfano wa kuigwa na kupongezwa. Vijijini sasa tunaona mashine za mazao na viwanda vinafunguliwa na hii inachangia kuimarika kwa uchumi wa wananchi wetu huko vijijini,” amesema Mhe. Mwassa.

Awali Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Nishati, Dkt. Khatib Kazungu amewashukuru Wabia hao wa maendeleo na kuongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana nao kuendelea kufikisha umeme vijijini ili lengo la kuwafikishia nishati bora wananchi wote, hata walio vijijini, linafikiwa.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali (mstaafu), Jacob Kingu amewashukuru Wabia wa Maendeleo kwa mchango wao katika Miradi ya kusambaza nishati vijijini na kuahidi yeye pamoja na Bodi yake kuendelea kuisimamia Menejimenti ya REA kuhakikisha mipango iliyopangwa inafikiwa na fedha zilizotengwa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Kwa niaba ya Mwenyekiti wa Wabia wa Maendeleo katika Sekta ya Nishati (EDPG), Morten Heide amesema kuwa wataendelea kushirikiana na Serikali kutekeleza miradi ya kupeleka nishati ya umeme vijijini ili kuendelea kuinua uchumi na kuboresha maisha ya wananchi waishio vijijini.

“Nishati ya umeme ni nishati muhimu sana katika maendeleo ya jamii yoyote duniani. Na sisi kama wabia tunaridhika na jitihada zinazofanywa kusambaza umeme katika vijiji na sasa katika vitongoji. Tunaahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kupeleka umeme vijijini na matumizi ya nishati safi ya kupikia,” amesema Heide.

Mkurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini, Mhandisi Hassan Saidy amesema kuwa wakala huo umeweza kufikia mafanikio ya kusambaza umeme vijijini kwa asilimia 99.5, ambapo vijiji 12,240 tayari vimefikiwa na umeme na kuongeza kuwa safari ya kupeleka umeme katika vitongoji imeanza.

“Mafanikio haya makubwa yamewezekana tuu kwa ushirikiano uliopo kati ya serikali yetu na wabia wa maendeleo ambao wamekuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha watanzania, hasa waishio vijijini, wanapata nishati bora ikiwamo nishati ya umeme,” amesema Mhandisi Saidy.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com