WAJASIRIAMALI WA NCHI WANACHAMA EAC WAHAMASISHWA KUWA WABUNIFU


Na: Mwandishi Wetu - Juba, Sudan Kusini

WAJASIRIAMALI wa Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wametakiwa kuhakikisha wanakuwa wabunifu na kuongeza ujuzi ili kutengeneza bidhaa zenye ubora zaidi.

Kauli hiyo imetolewa Jana Novemba 3, 2024 na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulrmavu, Zuhura Yunus wakati akizungumza kwenye Maadhimisho ya Siku ya Tanzania iliyofanyika tarehe 3 Novemba, 2024 jijini Juba, Sudan Kusini ikiwa ni sehemu ya shughuli za Maonesho ya 24 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu Nguvu Kazi au Jua Kali yanayoendelea jijini humo yakiongozwa na kauli mbiu isemayo, "Kukuza Ubunifu wa Kipekee na Maendeleo ya Ujuzi miongoni mwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Afrika Mashariki."

Aidha, Naibu Katibu Mkuu Zuhura Yunus amesema kuwa kauli mbiu ya maonesho hayo inahamasisha nchi wanachama wa jumuiya hiyo kutambua na kuthamini suala la kukuza na kuongeza ujuzi na ubunifu kwa wajasiriamali ili kuongeza tija na faida katika utengenezani wa bidhaa zao.

Vile vile, Naibu Katibu Zuhura Yunus ameitaka Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuendelea kuyapa kipaumbele maonesho hayo ya ambayo yamekuwa chachu kwa Wajasiriamali Wadogo na wa Kati kukua kibiashara na kutangaza bidhaa zao.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Fedha na Biashara, Annette Mutaawe amesema maonesho hayo yameendelea kuwawezesha wajasiriamali kuongeza uwezo kibiashara na kupanua wigo wa masoko yao kikanda.

Naye, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wajasiramali Wadogo na wa Kati EAC (CISO), Josephat Rweyemamu amesema maonesho hayo yamekuwa yakiwavutia Wajasiriamali wengi wa Tanzania kushiriki kwa katika maonesho hayo.

Wajasiriamali walioshiriki katika maonesho hayo wamesema wameweza kutangaza bidhaa zinazozalishwa nchini Tanzania na wameishukuru Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha ushiriki wao.

Maonesho hayo ya 24 yamewashirikisha wajasiriamali 1,700 kutoka nchi zote wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, wakiwemo 299 kutoka Tanzania na yanafanyika kwa mara ya kwanza nchini Sudan Kusini tangu nchi hiyo ijiunge katika jumuiya hiyo mwaka 2016.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post