WMA YASISITIZA MATUMIZI SAHIHI YA VIPIMO KWA WAUZAJI WA MVINYO


Wakala wa Vipimo (WMA) Mkoa wa Dodoma imewahimiza wajasiriamali na wafanyabiashara wanaojihusisha na uuzaji wa mvinyo na usindikaji wa bidhaa zinazotokana na zao la zabibu kuzingatia matumizi sahihi ya vipimo katika biashara zao.

Wito huo umetolewa na Meneja wa WMA Mkoa wa Dodoma Bw. Karim Zuberi alipowatembelea wauzaji wa mvinyo wanaoshiriki katika Tamasha la Dodoma Zabibu Tourism International Fair kwenye Viwanja vya Reli Dodoma Mjini ambapo WMA ni moja ya taasisi shiriki katika tamasha hilo.

Akifafanua zaidi Bw. Zuberi amesema kuwa mkoa wa Dodoma unaongoza kwa kilimo cha zao la zabibu nchini ambapo zao hilo ni moja kati ya mazao ya kimkakati hivyo amewataka wakulima na wafanyabiashara kujikita katika uzalishaji wenye tija kwa kuhakikisha zabibu zinazofungashwa na kuuzwa kwenye maduka mbalimbali na zile zinazo safirishwa kwenda nchi jirani zinapimwa na kufungashwa kwa kuzingatia vipimo sahihi, na wale wanaoongeza thamani kwa kutengeneza mvinyo kadharika wafungashe kwa kutumia vipimo sahihi ili kuwalinda walaji.

“Katika Jiji letu la Dodoma wafanyabiashara wengi huliongezea thamani zao la zabibu kwa kutengeneza mvinyo (wine) na hufungashwa kwenye madumu na chupa zenye ujazo tofauti hivyo nawaasa wafanyabiashara kutumia vipimo sahihi katika uzalishaji wao kama ambavyo Sheria ya Vipimo Sura Na.340 inavyoelekeza.”

“Mkishatumia Vipimo sahihi katika kufungasha bidhaa hii ya mvinyo, hakikisheni mmeweka alama ya maandishi au kibandiko chenye kuonesha ujazo wa mvinyo katika kifungashio husika. Hii itachagiza kuleta haki baina ya muuzaji na mnunuzi kwa kujua kiasi sahihi cha bidhaa anayonunua” ameongeza Bw. Zuberi.

Sanjari na hayo Meneja Zuberi amewakaribisha wananchi wa Mkoa wa Dodoma kutembelea banda la WMA katika maonesho hayo ili kuendelea kujifunza juu ya huduma zinazotolewa na Wakala ikiwa ni pamoja na eneo la uhakiki wa dira za maji mpya pamoja na zile ambazo zipo kwenye matumizi, mita za umeme na vipimo vingine.

Kwa upande wake mjasiriamali wa bidhaa ya mvinyo Bi. Zaituni Ramadhani ameishukuru WMA kwa kutembelea bidhaa zake na kumpa ushauri wa kitaalamu wa namna ya kuboresha ufungasaji wa bidhaa zake ikiwa ni pamoja na kuweka taarifa za kiujumla juu ya ufungashaji wa bidhaa yake.

Wakala wa Vipimo imeendelea na uboreshaji wa huduma zake kwa kutimiza majukumu yake kwa ufanisi na kushirikiana na wadau wa vipimo pamoja na wananchi kwa ujumla kwa kushiriki katika maonesho, hafla na mikutano mbalimbali yenye tija katika kuinua sekta ya vipimo nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post