Kamati ya wataalamu wa masuala ya Habari Zanzibar (ZAMECO) inayoundwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA- Zanzibar), Baraza la Habari Tanzania (MCT), Jumuiya ya Waandishi wa Habari za Maendeleo Zanzibar (WAHAMAZA), Jukwaa la Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC Zanzibar) , Klabu ya Waandishi wa Habari Zanzibar (ZPC) pamoja na Klabu ya Waandishi wa Habari Pemba (PPC) imelaani video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii ikionesha wasichana wawili wakirekodiwa na kuulizwa maswali yasio na maadili na yenye kuvunja heshima na haki za binaadamu.
Tukio hili limeibua hisia kali kwa wadau wa habari, watetezi wa haki za binaadamu na jamii kwa ujumla na kuibua maswali yasio na majibu miongoni mwa wanahabari kuhusu maadili, haki za binadamu, na misingi ya uhuru wa vyombo vya habari.
Hivyo basi ZAMECO inasisitiza kuwa vitendo vya udhalilishaji kwa watoto wa kike na jamii kwa ujumla ni ukiukwaji wa haki za binaadamu, maadili ya uandishi wa habari, na kuvuruga mipaka ya uhuru wa kujieleza ambapo unalindwa na unahitajika kwa lengo la kutoa habari sahihi na kuibua mijadala yenye tija na manufaa kwa jamii.
Kwa mujibu wa Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR 1996) Ibara (19) "Kila mtu ana uhuru wa kutoa taarifa bila ya kuathiri haki ya mtu na amani ya nchi,” hii ina maana kuwa uhuru wa vyombo vya habari unaendana na jukumu la kuheshimu utu wa kila mtu, hasa wanawake na vijana, ambao ni waathirika wa moja kwa moja katika hatari yoyote itakayotokea.
ZAMECO inatoa msisitizo kwa mamlaka husika (Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) pamoja na Tume ya Utangazaji Zanzibar kuhakikisha maudhui yanayorushwa na vyombo vya habari na mitandao ya kijamii yanaendana na viwango vya maadili, uwajibikaji na kuhakikisha kulinda jamii dhidi ya maudhui yenye madhara kwao, kama vile yaliyomo yanayokiuka haki za binadamu, kudhalilisha, au kuchochea vurugu na chuki.
ZAMECO pia inaiomba Wizara ya Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo Zanzibar kuharakisha upatikanaji wa Sheria mpya ya Huduma za Habari nchini kwa lengo la kupunguza changamoto kama hizo kwani ukizingatia katika mapendekezo ya sheria hiyo (ambayo ni kilio cha muda mrefu kwa waandishi, wahariri na jamii kwa ujumla) imeelezea kwa kina nani muandishi wa habari, sifa zake na kazi zake kwa ujumla.
Sambamba na hilo kamati ya wataalamu wa habari inatoa wito kwa mamlaka husika kuchukuliwa hatua stahiki wale wote waliohusika kutengeza na kusambaza video hizo zinazoharibu maadili haki za binadamu, na misingi ya uhuru wa vyombo vya habari katika mitandao ya kijamii.
Aidha Kamati hiyo inasisitiza umuhimu wa wasichana kujitambua, kujithamini, na kujiwekea malengo ambayo yatasaidia kuboresha maisha yao na jamii kwa ujumla kwani wasichana wanapojitambua, wanakuwa na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi, kujiamini, na kuepuka kutumiwa kwa maslahi ya wengine ambayo yanaweza kudhoofisha ndoto zao.
ZAMECO pia inawaomba wazazi na walezi kuwa mstari wa mbele katika kuwaelimisha watoto wao wa kike juu ya thamani yao, haki zao, na nafasi yao katika jamii “ukimuelimisha mtoto wa kike ni sawa na kuielimisha jamii, sambamba na kuwaelimisha vijana wa kiume kuwaheshimu watoto wa kike kwa kuwajengea mazingira yenye maadili na heshima Kamati ya wataalamu wa masuala ya Habari Zanzibar.
ZAMECO ipo tayari kushirikiana na wadau wa sekta ya habari na Watetezi wa haki za binaadamu kuhakikisha kuwa matukio kama haya hayajirudii tena, na kila mwandishi wa habari, mhariri, na mtangazaji wanaelewa na kutekeleza majukumu yao kwa njia inayolinda heshima, utu wa binadamu na maadili ya uandishi wa habari.
Mwenyekiti ZPC......................................Abdalla Mfaume
Mkurugenzi TAMWA-ZNZ ..................... Dr. Mzuri Issa
Social Plugin