●Serikali yakusanya Sh.Bilioni 325 ndani ya miezi mitano
Msigwa amesema kuwa, matunda ya Uwekezaji wa DP World katika Bandari ya Dar es Salaam yameanza kuonekana ambapo katika kipindi cha miezi mitano tangu ianze kuendesha Bandari hiyo, Serikali ya Tanzania imekusanya Shilingi. Bilioni 325.
Akiongea Jijini Dar es Salaam Disemba 19,2024, Msigwa amesema, Serikali imeanza kuona matunda matamu ya DP World ndani ya kipindi kifupi sana, tangu kampuni ya DP World Dar es Salaam ianze uendeshaji katika Bandari ya Dar es Salaam mwezi Aprili 2024, tumepata mafanikio makubwa.
Ameyataja mafanikio hayo kwa mujibu wa mkataba kampuni ya DP World ambayo kwetu Tanzania inakuwa DP World Dar es Salaam inapaswa kuwekeza Dola za Marekani Milioni 250 sawa na Shilingi Bilioni 675 katika kipindi cha miaka mitano, na kwamba katika kipindi cha miezi mitano tu tayari kampuni hii imeshawekeza Shilingi Bilioni 214.425 na hii ni sawa na 31% ya uwekezaji tuliotarajia katika kipindi cha miaka mitano.
“Maana yake huko nyuma kulikuwa na maneno tumeweka Wasanii sijui nini watakuja sasa hapa kwa lugha ya Kikinga 'we mean ' business na tutasimamia mkataba huu kuhakikisha maslahi ya Watanzania yanalindwa” amesema Msigwa.
Ameongeza kuwa, ukarabati wa mitambo iliyokuwa ya TPA imefanyika na usimikaji wa mifumo ya TEHAMA ya uendeshaji wa Bandari umefanyika, sasa manufaa mengine ambayo wakati ule yalikuwa yakiimbwa sana na kuitwa Wasanii na mambo mengine mengi.
“Wastani wa muda wa meli kusubiri wakati ule meli zetu zilikuwa zinasubiri siku 46 nyingine hadi siku 70 lakini sasa hivi meli zinasubiri kwa siku 7 maana yake tunapunguza gharama ambazo Serikali kupitia TPA imekuwa ikiwalipa wenye meli kutokana na meli zao kusubiri muda mrefu kushusha mizigo, na hiyo ni wastani lakini zipo meli hazisubiri kabisa, meli za makasha hakuna kusubiri zikija zinashusha zinaondoka,” ameongeza.
Serikali inaendesha Bandari kwa faida, ambapo hapo awali ilikuwa inaendeshwa kwa hasara, katika kipindi cha miezi mitano tangu DP World waanze kazi Serikali imefanikiwa kukusanya Shilingi Bilioni 325.3 ikiwa ni mapato yanayotokana na shughuli za mikataba iliyoingia kati ya TPA na DP World.
Social Plugin