Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VIONGOZI WA KATA YA MJIMWEMA SONGEA WAJIPANGA KUKAMILISHA MIRADI YA ELIMU KABLA YA JANUARI 2025


Diwani wa Kata ya Mjimwema, Silvester Mhagama akizungumza kwenye kikao

Na Regina Ndumbaro - Ruvuma.

Viongozi wa Kata ya Mjimwema, iliyopo Manispaa ya Songea, Mkoani Ruvuma, wamejipanga kuhakikisha miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa vyumba vya madarasa na vyoo, inakamilika kwa wakati, ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa vyumba vya madarasa pindi shule zitakapofunguliwa Januari 2025.

Katika kikao cha pamoja kilichoshirikisha viongozi wa mitaa ya kata hiyo na watumishi kutoka Kituo cha Afya Mjimwema, Diwani wa Kata ya Mjimwema, Silvester Mhagama, ameeleza kuwa mikakati inayoandaliwa ni kuhakikisha kwamba miradi hiyo inatekelezwa kwa ufanisi.

Aidha amesisitiza umuhimu wa kukamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa na matundu ya vyoo haraka lengo kuu ni kuepuka upungufu wa miundombinu wakati wa ufunguzi wa shule mwaka 2025.

Naye Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Mjimwema, Dkt. Alice Kitiri, ametumia nafasi hiyo kuhimiza jamii kujenga mshikamano katika kutunza mazingira na kuzingatia usafi ili kuepusha magonjwa ya milipuko. 

Dkt. Kitiri ameshauri akina mama kutembelea vituo vya afya mapema wakati wa ujauzito ili kupata huduma za afya kwa wakati na hivyo kupunguza hatari ya matatizo ya uzazi kwa mama na mtoto.

Viongozi hao wamekubaliana kuwa hatua hizi ni muhimu kwa ustawi wa jamii ya Mjimwema, na kuahidi kufanya kila juhudi kuhakikisha utekelezaji wa miradi hiyo unafanikiwa kwa wakati na kwa kiwango cha juu cha ubora.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com