Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SHUWASA YAANZA KUPANUA MTAMBO WA KUCHAKATA TOPE KINYESI ILI KUBORESHA HUDUMA ZA USAFI SHINYANGA

Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Shinyanga (SHUWASA) inaendelea na utekelezaji wa mradi wa kupanua mtambo wa kuchakata tope kinyesi, lengo likiwa ni kuboresha huduma za usafi na kukidhi mahitaji ya wananchi wa Manispaa ya Shinyanga.

Mtambo huo, uliopo katika Kata ya Kizumbi, Manispaa ya Shinyanga, awali ulikuwa na uwezo wa kuchakata lita 40,000 za tope kinyesi, lakini kupitia upanuzi unaoendelea, utaongezwa uwezo wa kuchakata hadi lita 100,000.

Meneja wa Uendeshaji na Miundombinu kutoka SHUWASA, Mhandisi Wilfred Lameck, ameeleza kuwa mradi huo umefikia asilimia 62 ya utekelezaji na unatarajiwa kukamilika kwa gharama ya Shilingi milioni 338.

"Lengo letu ni kuongeza wigo wa huduma na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za usafi, huku tukiendelea na juhudi za kuboresha miundombinu ya maji na usafi wa mazingira," amesema Mhandisi Lameck.

Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA, Mhandisi Yusuph Katopola, amebainisha kuwa mtambo huu ulianza kwa ushirikiano na Shirika la Maendeleo la Uholanzi (SNV) pamoja na Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, na umekuwa na manufaa kwa zaidi ya wananchi 200,000 wa manispaa na miji jirani.

Kwa upande wake, Mkandarasi wa mradi, Bw. Swalehe Maganga kutoka Kampuni ya Kanuta Engineering Supply, aliahidi kumaliza mradi kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa, kuhakikisha kuwa fedha za umma zinatumika ipasavyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa SHUWASA Mhandisi Yusuph Katopola akielezea kuhusu utekelezaji wa mradi wa kupanua mtambo wa kuchakata tope kinyesi

Meneja uendeshaji miundombinu kutoka SHUWASA Mhandisi Wilfred Lameck akizungumzia utekelezaji wa mradi wa kupanua mtambo wa kuchakata tope kinyesi
Meneja uendeshaji miundombinu kutoka SHUWASA Mhandisi Wilfred Lameck akizungumzia utekelezaji wa mradi wa kupanua mtambo wa kuchakata tope kinyesi
Mkandarasi Swalehe Maganga kutoka Kampuni ya Kanuta Engineering supply, akielezea kuhusu utekelezaji wa mradi wa kupanua mtambo wa kuchakata tope kinyesi
Gari likimwaga Majitaka kwenye Mtambo uliopo sasa wa kuchakata Tope Kinyesi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com