Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linahamasisha wananchi kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu msimu huu wa sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, ili kuimarisha usalama katika jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Desemba 23,2024 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, amesisitiza kuwa ushirikiano wa wananchi na vyombo vya usalama ni muhimu katika kupambana na uhalifu na kuhakikisha kuwa mazingira ya sherehe yanakuwa salama kwa kila mmoja.
Ameongeza kuwa katika kipindi hiki cha sikukuu, kuna hatari ya wahalifu kutumia fursa ya msimu huu kufanya uhalifu, hivyo ni muhimu kila mtu kuwa macho na kutoa taarifa kwa wakati.
Kamanda Magomi ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu, na pia amekumbusha wazazi na walezi kuwa makini na watoto wao katika kipindi hiki cha sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, ili kuhakikisha kuwa usalama unadumishwa na kila mmoja anapata fursa ya kufurahi na kusherehekea kwa amani.
Katika hatua nyingine, Kamanda Magomi ameeleza mafanikio ya misako na operesheni mbalimbali zilizofanyika kuanzia Novemba 27, 2024 hadi Disemba 22, 2024, ambapo Jeshi la Polisi limefanikiwa kukamata wahalifu na vielelezo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na silaha aina ya Gobore, madini bandia, pombe ya moshi, na pikipiki.
Katika operesheni hiyo, watuhumiwa 81 walikamatwa na vifaa mbalimbali vilivyohusiana na uhalifu, ikiwa ni pamoja na madini bandia gramu 250 yadhaniwayo kuwa ni Dhahabu, Bhangi gramu elfu 9, Mirungi bunda 09, Pombe ya moshi lita 113, Sola panel 07, Betri 04 za Sola, Pikipiki 11, Kadi 03 za Pikipiki, Antena 04 za ving'amuzi, Simu 03, Redio 02, Baiskeli 02, Mashine ya Bonanza 01, Kamera 01, na Mitambo 04 ya kutengeneza pombe ya moshi.
Kamanda Magomi pia ametangaza mafanikio ya kesi mahakamani, ambapo jumla ya kesi 18 zimepata mafanikio, na washitakiwa wameshapatikana na adhabu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kifungo cha maisha jela kwa washitakiwa wanne wa unyang'anyi wa kutumia silaha.
Aidha, kesi nyingine zimehusisha makosa ya kubaka, kumlawiti, kumiliki nyara za serikali kinyume na sheria, dawa za kulevya, wizi, na uvunjaji wa nyumba, ambapo washitakiwa wamehukumiwa kifungo cha kati ya miezi mitatu hadi miaka 30 jela.
Kwa upande wa operesheni za usalama barabarani, Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga limefanikiwa kukamata jumla ya makosa 5,376, ambapo makosa ya magari yalikuwa 3,767 na makosa ya bajaji na pikipiki yalikuwa 1,609.
Wahusika walilipa faini za papo kwa hapo.
Jeshi la Polisi pia limeendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu kupinga ukatili wa kijinsia, ulinzi shirikishi, na usalama barabarani, na limezindua kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia.
Social Plugin