Mtafiti wa Dawa aina ya Lab spray Disinfectant Mwalimu Ally Issa akiwa katika Banda la VETA linalopatikana katika Maonyesho ya Tisa ya sayansi,Teknolojia na ubunifu (STICE) yaliyoandaliwa na COSTECTH akionyesha Dawa hiyo.
Na Hellen Kwavava - Dar Es Salaam
MAMLAKA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (VETA), imegundua dawa ya kukabiliana na ugonjwa ya maambukizi ya bakteria kwa njia ya mkojo (UTI) na fangasi inayoitwa Lab Spray Disinfectant.
Hayo aliyasema Mwalimu wa Maabara , Ally Issa jana katika Kongamano na maonyesho ya tisa ya Sayansi, Teknolojia, na Ubunifu (STICE).
Alisema bakteria wengi wa magonjwa hayo hupatikana kwenye vyoo vinavyo patikana kwenye Mkusanyiko wa watu (UMMA)hivyo, inatakiwa kabla ya kutumia choo unapulizia dawa hiyo kisha unatumia.
"Kama unasumbuliwa na fangasi kwenye miguu unachukua dawa hii na kuipulizia kwenye eneo lililoathirika. Dawa hii imetengenezwa na Glycerin, Ethanol, Benzoic na Salicylic kwa ajili ya kuua bakretia wa UTI na fangasi," alieleza.
Mwalimu Issa aliendelea kwa kusema kuwa dawa hiyo ina ujazo wa mililita 120 na kuuzwa kwa Sh 4,000 na inapatikana kwenye vyuo hivyo.
Aidha alieleza kuwa kitengo hicho kimetengeneza mafuta ya mwarobaini kwa ajili ya kujikinga na kudhibiti mbu.
Hata hivyo alisema mafuta hayo yametengenezwa kwa utaratibu maalum kwa kutumia majani ya mwarobaini, mchaichai na mafuta ya nazi.
"Mafuta haya hayana kemikali yoyote kwa sababu yametengenezwa na vitu asili. Ukiyapaka mwilini hakuna mbu atakayekusogelea," alisema Issa.
Alisema kuwa chuo hicho cha Veta kinatoa kozi ya maabara kwa vyuo vinne vya Veta Dar es Salaam, Mtwara, Pwani na Manyara na kwamba lengo la kozi hiyo ni kumuandaa mwanafunzi kuwa mtaalamu wa kuzalisha bidhaa mbalimbali, kupima na kuzingatia ubora na viwango vinavyotakiwa.
Kupitia kozi hiyo wametengeneza mbolea inayotokana na majani ya maharage kwa ajili ya kilimo na mbolea itokanayo na mazao ya baharini ili kuchochea uchumi wa buluu.
"Tunataka vijana wawe na mawazo bunifu ambayo yatasaidia kutatua changamoto katika jamii hivyo, kuzalisha ajira na kupata kipato kitakachowasaidia kujikwamua kimaisha," alisema Issa.
Social Plugin