Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WACHIMBAJI WADOGO BUGARAMA WAOMBA UWEZESHAJI WA VIFAA VYA KAZI KWA SERIKALI

Wachimbaji wadogo wa madini kutoka kijiji cha Bugarama, kata ya Bugarama, Halmashauri ya Msalala, wilaya ya Kahama, mkoa wa Shinyanga, wameomba msaada wa kifedha na vifaa vya kazi ili kuboresha shughuli zao za uchimbaji na kujikwamua kiuchumi.

Akizungumza na Malunde 1 blog, Mwenyekiti wa Kikundi cha Wachimbaji Wadogo Bugarama, Ezekiel Makoye Mageleja, amesema kuwa kwa sasa wanakikundi wanakutana na changamoto kubwa ya uchimbaji kwa kutumia vifaa duni na mtaji mdogo.

 Ameongeza kuwa, kutokana na hali hiyo, wanapata mapato kidogo ambayo yanatosha kujikimu tu na si zaidi.

"Tunaomba msaada kutoka kwa serikali ili tupate vifaa muhimu kama vile crusher (kifaa cha kusaga mawe), bambam (kifaa cha kuimarisha udongo na kuondoa mawe makubwa), pamoja na generator kwa ajili ya umeme. Hii itatusaidia kuongeza uzalishaji na kuboresha shughuli zetu za uchimbaji," amesema Makoye.

Aidha, amesema kuwa wanahitaji kiasi cha shilingi milioni 14 (14,000,000) kwa ajili kuendeshea shughuli zao kwa ufanisi. 

Makoye amesisitiza kuwa, msaada huu utaleta mabadiliko makubwa katika jamii yao kwa kutoa ajira kwa vijana na kuimarisha uchumi wa familia zao.

"Tulikuwa tukichimba kwa dhana duni na hatukuwa na mtaji wa kutosha. Hivyo, tunahitaji msaada huu ili kuweza kujikwamua na kuleta manufaa zaidi kwa jamii yetu," ameeleza Mwenyekiti huyo.

Wachimbaji hao wameomba serikali kupitia Wizara ya Madini kuzingatia ombi lao na kuwatengenezea mazingira bora ya kazi ili waweze kujikwamua na kuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa taifa.

Wasiliana na Ezekiel Mageleja Makoye kwa simu namba 0783 860 216

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com