Muonekano wa sehemu ya Mto Mhumbu Manispaa ya Shinyanga(Picha Maktaba Malunde 1 blog)
***
Mwanamke mmoja aliyefahamika kwa jina la Leah George (Nkwimba) mwenye umri wa miaka 44, mkazi wa mtaa wa Dome Kata ya Ndembezi katika Manispaa ya Shinyanga, anahofiwa kufa maji baada ya kusombwa na maji katika daraja la Machimu lililopo mtaa wa Tambukareli mjini Shinyanga linalopeleka maji mto Mhumbu
Tukio hilo limetokea jana majira ya saa moja jioni, baada ya mvua kubwa zilizonyesha katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Shinyanga na kusababisha baadhi ya madaraja kufunikwa na maji.
Kwa mujibu wa Mama mzazi wa Leah Bi. Rachel Faustine (72) mwanaye aliondoka jana asubuhi na kwenda mtaa wa Tambukareli kwa shughuli zake, lakini hakurudi mpaka leo asubuhi alipopigiwa simu na kuelezwa kuwa amesombwa na maji katika daraja hilo, wakati akijaribu kuvuka kurudi nyumbani baada ya mvua kukatika.
Amesema baada ya kupata taarifa hizo alishirikiana na majirani kuwataarifu viongozi wa mtaa, ambapo Mwenyekiti wa Mtaa huo alifika na kutoa taarifa kwa Jeshi la Zimamoto na uokoaji ambalo lilifika eneo la tukio na kuanza kuutafuta mwili wa Leah bila mafanikio.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Dome Bw. Solomon Nalinga Najulwa amebainisha kuwa, juhudi za kuutafuta mwili wa Leah zilizokuwa zikifanywa na Jeshi la Zimamoto na uokoaji kwa kushirikiana na wananchi zimeshindikana kwa siku ya leo na kwamba, zoezi hilo litaendelea tena kesho asubuhi.
Najulwa amewataka wananchi kuchukua tahadhari katika kipindi hiki cha mvua kwa kutojaribu kuvuka kwenye mito au madaraja yaliyofunikwa na maji, kwa kuwa jambo hilo linahatarisha maisha.
Aidha, amewataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto wao hawavuki au kutembea peke yao kwenye maeneo yenye maji mengi katika kipindi hiki cha mvua, ikiwemo kuwaongoza wakati wa kwenda na kurudi shule.
Chanzo - Radio Faraja
Social Plugin