Na Regina Ndumbaro - Ruvuma
Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea, Ndugu Simoni Kapinga, amemuwakilisha Mheshimiwa Jenista Mhagama, Mbunge wa Songea Vijijini na Waziri wa Afya, katika kukabidhi gari la wagonjwa kwa Kituo cha Afya cha Muhukuru kilichopo katika Wilaya ya Songea Vijijini.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Ndugu Kapinga amewahimiza wananchi wa Kata ya Muhukuru kutumia gari hilo pindi panapozuka dharura za kitabibu.
Amesema gari hili litasaidia katika kusafirisha wagonjwa wanaohitaji huduma za haraka, hususan akina mama wajawazito na watoto, wanaohitaji kufikishwa kwenye hospitali kubwa ya mkoa.
Kwa upande wake, Dkt. Emanuel Tandewa, Daktari wa Kituo cha Afya cha Muhukuru, ameelezea historia fupi ya kituo hicho kilichozinduliwa mwaka 1968.
Amesema changamoto kuu wanayokutana nayo ni ukosefu wa gari la wagonjwa, jambo ambalo limekuwa likiwawia vigumu akina mama wajawazito na watoto kupata usafiri wa haraka.
Dkt. Tandewa ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa juhudi zake, hasa kwa kumteua Mheshimiwa Jenista Mhagama kuwa kiongozi ambaye ameonyesha uthubutu na kujitolea kwa ajili ya wananchi wenye uhitaji.
Aidha, Dkt. Tandewa ametoa wito kwa viongozi wengine kujitokeza na kujitolea kwa hali na mali katika kuboresha huduma za kijamii, hususani katika vituo vya afya na shule, ili kuhakikisha maendeleo ya huduma za afya na elimu kwa wananchi wa maeneo ya vijijini.
Hii ni juhudi muhimu katika kuboresha huduma za afya na kuhakikisha kuwa wananchi wa Kata ya Muhukuru wanapata huduma bora za afya kwa wakati.
Social Plugin