Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inatarajia kuuza gramu 184.06 za madini mbalimbali ya vito yenye thamani inayokadiriwa kufikia Shilingi Bilioni 3.1 kupitia mnada, katika mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro, Mkoa wa Manyara.
Mnada huo wa kwanza wa ndani wa madini ya vito, unaendeshwa kwa njia ya Kidijitali, ambayo imetoa nafasi kwa wafanyabiashara wa Madini kutoka maeneo mbalimbali nchini kushiriki kwa njia ya mtandao.
Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amekuwa mgeni rasmi kwenye mnada huo wa Madini ya vito, mnada ambao ulisimama kwa muda na hatimae kuzinduliwa Disemba 14, 2024, katika Mji mdogo wa Mirerani.
Mavunde amesema, utaratibu wa kufanya mnada huo ni jitihada za Serikali za kudhibiti utoroshwaji wa madini hayo nje ya nchi na pia kuwasaidia wachimbaji kuuza madini yao kwa bei ya ushindani inayoendana na Soko la Dunia.
“Serikali imedhamiria kudhibiti utoroshwaji wa Madini, lakini pia kuuza kwa njia ya mnada itasadia kuyaongezea thamani ambapo madini yanafanyiwa mnada kama mkakati wa kuyatangaza na kuyaongezea thamani Kimataifa, amesema Waziri Mavunde.
Awali alipotoa taarifa ya mnada huo, Waziri Mavunde ameeleza kuwa, mnada huo utashirikisha wanunuzi kutoka ndani na nje ya nchi na atakayenunua madini hayo katika mnada ni atakayeshinda bei iliyowekwa.
Mnada huu utaendeshwa kwa usalama mkubwa kwa kuwa madini hayo hususan Tanzanite yana thamani kubwa. Serikali imeimarisha ulinzi ili kujihadhari na watu wasio waaminifu,”amesema Waziri Mavunde.
Aidha, amesema mnada huo utaiwezesha Serikali kupata mrabaha stahiki na kodi kwa uwazi ili kuchangia pato la Taifa na kuimarisha ulinzi na usalama kwa wauzaji, wanunuzi na mali zao.
Minada kama hiyo pia hufanyika kwa nchi za Afrika zenye madini ya vito kama vile Zambia (emerald), Zimbabwe (almasi) na Afrika Kusini (almasi).