Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

INEC YATANGAZA RATIBA YA UBORESHAJI WA DAFTARI LA KUDUMU LA WAPIGA KURA MIKOA YA RUVUMA, NJOMBE, SONGWE NA RUKWA

Na Regina Ndumbaro - Ruvuma 

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza ratiba ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura kwa mikoa ya Ruvuma, Njombe, Songwe, na Rukwa. Zoezi hilo litaanza tarehe 12 Januari 2025 na kumalizika tarehe 18 Januari 2025. 

Lengo kuu ni kuandikisha wapiga kura wapya, na jumla ya wapiga kura wapya 475,743 wanatarajiwa kuandikishwa katika mikoa hiyo.

Akizungumza katika mkutano ya Tume na wadau wa uchaguzi uliofanyika tarehe 31 Desemba 2024, Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji wa Mahakama ya Rufaa, Mhe. Jacobs Mwambegele, kupitia kwa Stanslaus Mwita, amesema mikoa hiyo itafanya uboreshaji katika mzunguko wa tisa. 

Ameongeza kwamba Tume tayari imekamilisha uboreshaji katika mikoa 19, ikiwa ni pamoja na mizunguko nane kati ya mizunguko 13 ambayo imepangwa kukamilisha zoezi hilo nchini.

Mikoa ya Ruvuma, Njombe, Songwe, na Rukwa ni miongoni mwa mikoa inayohusishwa na uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. 

Mwita ametaja mikoa mingine ambayo tayari imekamilisha zoezi hilo kuwa ni Kigoma, Tabora, Katavi, Geita, Kagera, Mwanza, Shinyanga, Mara, Simiyu, Manyara, Dodoma, na Singida.

 Vilevile, amesema mikoa ya Zanzibar ikiwa ni Mjini Magharibi, Kusini Unguja, Kaskazini Unguja, Kusini Pemba, na Kaskazini Pemba, pamoja na mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, pia imekamilisha zoezi hili. 

Mikoa ya Mbeya na Iringa inatarajiwa kukamilisha zoezi hilo tarehe 2 Januari 2025.

Baada ya uboreshaji, mikoa ya Ruvuma, Njombe, Songwe, na Rukwa inatarajiwa kuwa na wapiga kura 3,091,485, ikilinganishwa na 2,615,742 waliokuwemo katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mwaka 2020. 

Idadi hii inaweza kuongezeka kutokana na uwepo wa Watanzania ambao walikuwa na sifa za kujiandikisha mwaka 2019/2020, lakini walikosa fursa ya kufanya hivyo.

Aidha, Tume imeongeza vituo vya kupigia kura kutoka 3,552 vilivyokuwepo mwaka 2020 hadi 3,785, ikiwa ni ongezeko la vituo 233.







Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com