Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

HALMASHAURI YA CHALINZE KUONGEZA ZAIDI UJENZI WA SHULE ZA UPILI



NA. ELISANTE KINDULU, CHALINZE.

HALMASHAURI ya Chalinze mkoa wa Pwani imedhamiria kuongeza shule za sekondari kutoka ngazi ya kata na kufika hadi vijijini na kwenye vitongoji.

Akizungumza na wazazi, walimu pamoja na kamati ya shule ya msingi Kibiki katika mkutano maalum, diwani wa kata ya Bwilingu katika halmashauri ya Chalinze mh. Nasser Karama aliyasema hayo alipokaribishwa kuzungumza  katika hadhira hiyo mwishoni mwa wiki hii.

Mh. Nasser alisema kata ya Bwilingu peke yake ambayo ipo ndani ya makao makuu ya Halmashauri ya Chalinze ina shule za sekondari za serikali nne huku sekondari zingine mbili zinatarajiwa kujengwa katika kata hiyo. 

"Tunatarajia kujenga shule ya sekondari katika eneo la Chalinze mzee kwa gharama ya shilingi milioni 573 kwa mfuko wa Serikali kuu na sekondari nyingine eneo la Koo kwa shilingi milioni 150 kwa mapato ya ndani", alisema Mh. Diwani.

Aidha Mh. Nasser amesema kuwa amefanya mazungumzo na shirika la  vision fund kusaidia ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa ya shule za msingi katika kata yake. 

Katika hatua nyingine Mh. Diwani ameipongeza shule ya msingi Kibiki kwa  kushika nafasi ya kwanza kwa shule za Serikali katika kata ya Bwilingu katika ufaulu wa darasa la saba katika mtihani wa Taifa wa mwaka huu.

Naye mwalimu mkuu wa shule hiyo, Bi. Magreth Kileo ametoa wito kwa wananchi kuchangamkia fursa ya kujenga maduka kuzunguka shule, na kusema kuwa, kwa kufanya hivyo kutasaidia uzio wa shule na pia shule kupata mapato yake.

Akifunga mkutano huo, kaimu mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo Bw. Hassan Mzee na mwenyekiti wa jukwaa la wazazi Bw. Shamba Msakamali wamewahimiza wazazi kuendelea kuchangia maendeleo ya elimu kwani Serikali haiwezi kufanya kila kitu.
DIWANI wa kata ya Bwilingu katika halmashauri ya Chalinze, Mh. Nasser Karama akisisitiza jambo.
Kaimu Mwenyekiti wa kamati ya shule, Hassan Mzee

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com