Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni, Sanaa na michezo Zanzibar Mhe. Tabia Mwita Maulid
akikagua kazi za BAKIZA kwenye kongamano LA 8 la Kiswahili mjini Wete
NA. ELISANTE KINDULU, WETE-PEMBA
WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni, Sanaa na michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Tabia Mwita Maulid ameliasa baraza ya Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) na lile la Tanzania Bara (BAKITA) kufanya Kazi kwa ushirikiano katika kusanifisha lugha ya Kiswahili ili kukilinda Kiswahili kisipoteze radha yake.
Mhe. Tabia ameyasema hayo alipokuwa akifungua kongamano LA 8 la kimataifa la baraza la Kiswahili Zanzibar (BAKIZA) lililofanyika katika ukumbi wa baraza la wawakilishi mjini Wete leo 17.12.2024.
Mhe. Waziri pia amewataka wataalam wa Kiswahili watumie fursa kubidhaisha Kiswahili katika nyanja za ukalimani, tafsiri, utunzi wa vitabu uandishi wa makala na kazi za Sanaa.
Akimkaribisha mgeni rasmi kuzungumza, Mwenyekiti wa BAKIZA Bi.Saade Said Mbarouk amewashukuru wadau mbalimbali kutoka Tanzania visiwani, Tanzania Bara, Afrika Mashariki na Dunia kwa ujumla kuja kushiriki kongamano la 8 la kimataifa la BAKIZA.
Kongamano hilo limehudhuriwa na Katibu Mtendaji wa BAKITA Bi. Consolata Mushi, Katibu Mtendaji wa BAKIZA Bi. Mwanahija Ali Juma, katibu mtendaji wa kamisheni ya Kiswahili Afrika Mashariki Bi. Caroline Assimwe , viongozi wa serikali, wahadhiri wa vyuo vikuu, wanahabari, wasanii, waalimu na wadau mbalimbali wa Kiswahili kutoka ndani na nje ya Zanzibar.
Social Plugin