Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

DKT. NDUMBARO ACHAGULIWA MWENYEKITI WA KAMATI MAALUM YA MAWAZIRI WA SHERIA YA UMOJA WA AFRIKA


Waziri wa Katiba na Sheria Nchini Tanzania Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amechaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza maalum la Mawaziri wa Sheria la Umoja wa Afrika kikao kilichowakutanisha Mawaziri, Mabalozi na Wataalamu katika sekta ya Sheria wa Umoja wa Afrika kikao kilichofanyika kuanzia tarehe 14 na kumalizika leo tarehe 22 Desemba, 2024 katika hotel ya Golden Tulip Zanzibar.

Akizungumza wakati akihitimisha kikao hicho kilichodumu kwa muda wa siku kumi Waziri wa Katiba na Sheria na Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Sheria wa Umoja wa Afrika kutoka Nchini Tanzania Mhe.Dkt. Damas Ndumbaro amewashukuru Wajumbe wa Baraza hilo kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Mawaziri wa Sekta ya Sheria kwa Nchi za Umoja wa Afrika.

"Tumeikubali heshima mliyotupatia Nchi ya Tanzania kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi.Tutafanya kazi kwa pamoja katika kuhakikisha Umoja wa Afrika unakuwa ni sehemu nzuri katika sekta ya Sheria na mfano bora katika utoaji Haki kwa miaka inayokuja." Alisema Ndumbaro.

Waziri Ndumbaro amesema kuwa, Kamati za ufundi za Wataalamu katika masuala ya Haki na Sheria ni Kamati muhimu katika Umoja wa Afrika ikiwemo kupitia nyaraka ambazo zinatokea katika Kamati za Wataalamu nyingine ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu kwa wakati na usimamizi wa Haki na kuwa makini katika kufanya maamuzi kwa kufanya kazi kwa pamoja ili kufikia maamuzi yenye tija.

Waziri Ndumbaro amewataka Viongozi waliochaguliwa wakiwemo Makamu Wenyeviti watatu waliochaguliwa na Katibu wa Kamati hiyo kuhakikisha kuwa wanaanza utekelezaji wa maazimio waliyokubaliana kwa kuunda timu itakayowawezesha kufikisha ajenda kwa vyombo vya maamuzi ili kuweza kutekeleza matakwa ya Umoja wa Afrika.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com