Jumamosi tarehe 14 Desemba 2024, jijini Arusha, Benki ya CRDB ilihitimisha fainali za CRDB Bank Supa Cup 2024, mashindano yaliyojumuisha michezo ya soka na netiboli, kwa timu zilizoundwa na wafanyakazi wa benki hiyo, yakiwa ni mashindano yenye mbwembwe na ushindani wa hali ya juu. Timu mbalimbali kutoka kanda tofauti za Tanzania zilishiriki katika fainali hizo ambazo zilileta burudani, mshikamano, na ushindani mkubwa.
Fainali hizo zilihudhuriwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Bw. Frank Mmbando, pamoja na viongozi mbalimbali wa Benki ya CRDB. Viongozi hao ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji, Abdulmajid Nsekela, Mkurugenzi wa CRDB Bank Congo, Jessica Nyachiro, Afisa Mkuu wa Fedha, Fredrick Nshekanabo, Afisa Mkuu wa Uendeshaji, Bruce Mwile, Afisa Mkuu wa Biashara, Boma Raballa na Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, Godfrey Rutasingwa.
Matokeo ya Soka
Katika mchezo wa kutafuta mshindi wa nafasi ya tatu, timu ya Ulipo Tupo FC kutoka Kanda ya Ziwa iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Boom Advance FC kutoka Kanda ya Kaskazini.
Fainali kubwa ya soka ilishuhudia timu ya iMbeju FC kutoka Kanda ya Pwani ikiibuka kidedea kwa ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Al Barakah FC kutoka Kanda ya Magharibi. Ushindi huu umeifanya iMbeju FC kutwaa ubingwa wa CRDB Bank Supa Cup 2024.
Matokeo ya Netiboli
Kwa upande wa netiboli, nafasi ya tatu ilichukuliwa na Lipa Hapa Queens kutoka Kanda ya Dar es Salaam baada ya kuwashinda Popote Inatiki Queens kutoka Kanda ya Kati kwa alama 50-45.
Fainali ya netiboli iliwaweka uso kwa uso iMbeju Queens kutoka Kanda ya Pwani na Ulipo Tupo Queens kutoka Kanda ya Ziwa. iMbeju Queens walifanikiwa kushinda kwa alama 45-39, na hivyo kutwaa ubingwa wa netiboli.
Zawadi na Tuzo
Mashindano haya yalihitimishwa kwa utoaji wa tuzo mbalimbali kwa washindi wa michezo yote, huku fedha taslimu, medali, na vikombe vikikabidhiwa kwa washindi kama ifuatavyo:
Soka
Mshindi wa Kwanza: iMbeju FC – TZS 13,000,000/=
Mshindi wa Pili: Al Barakah FC – TZS 9,000,000/=
Mshindi wa Tatu: Ulipo Tupo FC – TZS 6,000,000/=
Netiboli
Mshindi wa Kwanza: iMbeju Queens – TZS 9,000,000/=
Mshindi wa Pili: Ulipo Tupo Queens – TZS 6,000,000/=
Mshindi wa Tatu: Lipa Hapa Queens – TZS 4,000,000/=
Tuzo Binafsi za Soka
Mchezaji Bora wa Mashindano (MVP): Godwin Edward Junye (iMbeju FC) – TZS 500,000/=
Mfungaji Bora: Abdallah Magoe (Ulipo Tupo FC) – TZS 500,000/=
Kipa Bora: Abbas Wadi Makame (iMbeju FC) – TZS 300,000/=
Mchezaji Bora wa Mechi ya Fainali: Stanislaus John Masaswe (iMbeju FC) – TZS 300,000/=
Tuzo Binafsi za Netiboli
Mchezaji Bora wa Mashindano (MVP): Ikutungangisya Richard (Ulipo Tupo Queens) – TZS 500,000/=
Mfungaji Bora: Saada Ally Juma (Lipa Hapa Queens) – TZS 500,000/=
Mchezaji Bora wa Mechi ya Fainali: Tumaini Ndosi (iMbeju Queens) – TZS 300,000/=
Akizungumza katika fainali hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alisema kuwa benki hiyo imeweka mikakati na sera mbalimbali za kuongeza chachu kwa wafanyakazi wake, na michezo ni mojawapo ya nyenzo muhimu katika kuhakikisha wanajenga umoja, afya njema, na furaha miongoni mwao.
"Mashindano ya CRDB Bank Supa Cup ni zaidi ya michezo; ni jukwaa la mshikamano, mawasiliano, na afya bora kwa wafanyakazi wetu. Tunajivunia kuona mshindano haya yakiendelea kuwa sehemu muhimu ya utamaduni wa Benki yetu," alisema Nsekela.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu, Godfrey Rutasingwa, alisisitiza umuhimu wa mashindano hayo katika kuongeza mshikamano miongoni mwa wafanyakazi. "Michezo huchangia kwa asilimia kubwa kuwaleta watu pamoja, na kupitia Supa Cup tumeweza kuona mshikamano wa kipekee kati ya wafanyakazi wetu kutoka kanda mbalimbali," alisema Rutasingwa.
Mashindano ya CRDB Bank Supa Cup 2024 yamehitimishwa kwa mafanikio makubwa, huku timu ya iMbeju kutoka Kanda ya Pwani iking'ara kwa kushinda vikombe vyote vya soka na netiboli. Shangwe na matarajio yameanza kuandaliwa kwa mashindano ya mwaka 2025, huku wafanyakazi na mashabiki wakiisubiri kwa hamu kubwa msimu ujao wa burudani.
Social Plugin