KATIBU wa NEC, Oganaizesheni, Issa Usi Gavu, ametoa wito kwa wanachama wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) kuendeleza umoja na mshikamano.
Amesema umoja waliouonyesha wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji wanapaswa kuuonyesha katika kipindi hichi kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika mwakani.
Gavu alitoa kauli hiyo leo mkoani Tanga wakati akizungumza na wajumbe wa baraza hilo ambapo aliipongeza jumuiya hiyo kwa mafanikio yaliyopatikana ikiwemo ongezeko la idadi ya wanachama.
"Pongezi kubwa kwa kuongeza idadi kubwa ya wananchama kutoka milioni 4.1 mpaka wanachama milioni 6.1. Maana yake kunaongezeko la wanachama takribani milioni mbili.
"Hivyo tuendelee kuongeza kasi ya usajili na kuhimiza wanachama wapya," ameeleza.
Pia, Gavu amesisitiza umuhimu wa kufuata miongozo na taratibu zilizowekwa na CCM kwa mujibu wa katiba.
"Chama chetu hakina shida ya watu kukipigia debe, kipo kamilifu, kina muundo na nyezo thabiti.
Amesisitiza: "Hatutoruhusu atokee mtu ninafsi awe yenye msemaji wa chama chetu, msemaji wa rais wetu."
"Tutaendelea kuwakumbusha kwamba hatukatai kushirikiana na mtu, kuchangiwa na mtu au kuambatana na mtu. Lakini anayetaka kutusaidia, kutuchangia lazima afuate miongozo na maelekezo yanayotokana na chama cha mapinduzi," ameeleza.
Kadhaloka, alitoa wito kwa jumuiya hiyo kuanza mikakati ya uimarishaji uchumi kwani ni njia pekee ya kukataa vikundi vyenye lengo la kuleta mpasuko.
Aidha, amesema uamuzi wa kufanyika mkutano wa jumuia hiyo mkoani Tanga, umeonyesha dhamira ya jumuiya hiyo katika kukiimarisha chama na jumuiya hiyo.
"Ni uamuzi mzuri, uamuzi sahihi wenye lengo la kuimarisha Chama na jumuiya zake ikiwa ni chachu ya kukiletea ushindi Chama Cha Mapinduzi," amesisitiza Gavu.
Amesema taarifa ya utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya jumuiya hiyo imeonyesha mafanikio makubwa.
Social Plugin