Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

JESHI LA POLISI DODOMA LASHAURI JAMII KUFANYA MATENDO YA HURUMA KWA WENYE MAHITAJI MAALUM







Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, kwa kushirikiana na Kundi la Wanawake na Samia na wadau wengine wa maendeleo, wamekuwa na juhudi kubwa za kusaidia jamii kwa kutoa msaada kwa wenye uhitaji,msaada huu umetolewa katika Kituo cha Upendo kilichopo Miyuji, ikiwa ni ishara ya kuleta tabasamu kwa watu wasiojiweza na kuonyesha mshikamano katika jamii.

Mkuu wa Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Eva Stesheni, amesema kuwa kitendo hicho ni kielelezo cha umuhimu wa jamii kushirikiana kwa pamoja kusaidia wahitaji.

Akizungumza kwa niaba ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, SACP George Katabazi, Stesheni ameeleza kuwa ni jukumu la kila mmoja katika jamii kusaidia wenye uhitaji, na kwamba Jeshi la Polisi linajivunia kuwa sehemu ya juhudi hizo za kijamii.
"Ziara hii inadhihirisha dhamira yetu kama Jeshi la Polisi kuwa sehemu ya jamii na kuchangia kwa njia mbalimbali, ili kusaidia jamii na kuleta tabasamu kwa watu wanaohitaji msaada," amesema ACP Stesheni.

Licha ya hayo, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuwa na moyo wa kusaidiana ili kuboresha maisha ya wale wanaohitaji msaada.

Amesema kuwa msaada wa kijamii kama huu ni muhimu katika kuhakikisha kuwa watu wanaoishi katika mazingira magumu wanapata huduma za msingi, kama vile chakula, mavazi, na huduma za afya.

ACP Stesheni ameeleza kuwa Jeshi la Polisi Mkoa wa Dodoma, kwa kushirikiana na makundi mbalimbali litaendelea kujitolea kwa kutoa misaada ya kihisani kwa wasiojiweza ili kupunguza changamoto wanazokutana nazo.

"Kama Jeshi la Polisi, tunaamini kuwa siyo tu jukumu letu kulinda amani na usalama, bali pia ni wajibu wetu kusaidia jamii, hasa kwa watu walioko katika mazingira magumu," anasisitiza.

Kaimu Msimamizi wa Kituo cha Upendo, Brother John Mbogo, mbali na kufurahishwa na msaada huo, amesema kuwa Kituo hicho kimejikita katika kutoa huduma za kijamii kwa watu wenye uhitaji ikiwa ni pamoja na yatima, watu wazima wenye ulemavu, na watoto wa mitaani.
Amesema kuwa msaada kutoka kwa Jeshi la Polisi na wadau wengine utasaidia kuboresha maisha ya watu walio katika mazingira magumu, na kwamba msaada huu umeleta faraja na matumaini kwa wahitaji.

"Leo tumeshuhudia upendo na mshikamano mkubwa kutoka kwa Jeshi la Polisi, Wanawake na Samia, pamoja na Scouts, ambao wameleta msaada mkubwa kwa wahitaji wetu hapa kituoni,kama Kituo cha Upendo, tunajivunia sana kushirikiana nanyi katika juhudi za kuboresha maisha ya watu hawa wenye uhitaji," alisema Brother Mbogo.

Ameeleza kuwa kituo hicho kimejizatiti kutoa huduma muhimu za kijamii ambazo zinajumuisha chakula, mavazi, elimu, na huduma za kiafya kwa watoto na watu wazima wanaoishi katika mazingira magumu.

Pia amesema kituo hicho kinawahudumia watu wengi ambao, bila msaada kutoka kwa watu wengine, wangeweza kukosa huduma muhimu za kila siku.

"Kituo chetu kimekuwa na mchango mkubwa katika maisha ya wasiojiweza, tunasaidia watu wenye ulemavu ambao wanahitaji huduma za afya, na watoto wa mitaani ambao wanahitaji makazi na uangalizi,msaada huu unaenda kutupunguzia baadhi ya changamoto zinazowakabili," amesema Brother Mbogo na kuongeza kuwa msaada huo umewaongezea moyo wa kuendelea kutoa huduma kwa watu walioko katika mazingira magumu.
Naye Mkuu wa wa kitengo cha Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Dodoma, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Christer Kayombo, amesema kuwa Kituo cha Upendo ni mfano bora wa jinsi huduma za kijamii zinavyoweza kuboresha maisha na kuwa kielelezo cha nguvu ya mshikamano huku akitumia nafasi hiyo kuwahimiza wanajamii kujitoa kusaidia kwa namna yoyote ile ili kujenga jamii bora na yenye mabadiliko.

"Kutoa ni moyo na sio utajiri, kila mtu ana uwezo wa kujitoa kulingana na hali yake ya maisha,tunahitaji kujitoa ili kusaidia kuboresha maisha ya watu na kuleta tabasamu kwa wale wanaohitaji msaada,kufanya matendo ya huruma ni ibada njema,tunaamini kuwa kama kila mmoja wetu atachangia kwa namna yake, jamii yetu itakuwa na maendeleo endelevu," amesema ASP Kayombo.

Pia, ASP Kayombo amesisitiza kuwa huduma za kijamii, kama zile zinazotolewa na Kituo cha Upendo, zinahitaji ushirikiano wa karibu kutoka kwa taasisi za kijamii na wananchi kwa ujumla.

 "Ushirikiano wa pamoja unaleta matokeo mazuri katika kufanikisha malengo ya kuleta mabadiliko chanya kwa walio katika mazingira magumu," ameongeza.

ASP Kayombo amehimiza wanawake na vijana kuwa mstari wa mbele katika kusaidia watu wenye uhitaji ambapo amesema kuwa kundi hilo ni nguzo muhimu katika jamii, na linapaswa kuwa na moyo wa huruma ili kuhakikisha kwamba jamii inaendelea kuwa na mafanikio.

"Wanawake na vijana ni nguzo muhimu katika jamii,tunataka kuona mabadiliko yanayoendelea kwenye jamii kwa manufaa ya taifa letu,nawashukuru wote ambao mmeshirikiana na Jeshi la Polisi katika msaada huu tunapaswa kujivunia na kuendeleza juhudi za kusaidia watu wenye uhitaji ,"amesisitiza.







Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com