Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga akizungumza wakati wa maadhimisho ya wiki ya ardhi yanayoendelea jijini Dodoma.
*********************
Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Anthony Sanga ameziagiza ofisi zote za Ardhi nchini kuanzia mkoa hadi halmashauri kuhakikisha zinakaa vikao vya muda mfupi kila asubuhi kabla ya kuanza kazi ili kuwa na njia bora ya kutatua changamoto za sekta hiyo.
Amesema, utaratibu wa kuwa na vikao vya muda mfupi kila siku asubuhi kutawawezesha watendaji hao wa sekta ya ardhi nchini kujua namna ya kushughulika na changamoto zinazojitokeza mara kwa mara katika maeneo yao ya kazi.
"Mnapokutana mnakaa kwanza vikao vifupi kila subuhi kabla ya kuanza kazi na kupanga mipango, hata kama kikao cha cha dakika tano ili kuona jana mlifanya kazi vipi na kuna changamoto gani ili mzishughulikie" amesema Mhandisi Sanga.
Katibu Mkuu Mhandisi Sanga ametoa maagizo hayo tarehe 2 Desemba 2024 katika ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Ardhi ambayo uzinduzi wake utafanyika rasmikesho jumanne tarehe 3 Desemba 2024.
Aidha, amewataka watendaji wa sekta ya Ardhi nchini kujitambua na kuelewa kuwa, watumishi wote wa sekta hiyo ni wamoja na wananchi wanaelewa kuwa wote ni watumishi wa Ardhi bila kuchanganua taaluma zao.
"Unapomuambia mwananchi ramani haijapanda yeye haelewi , usimtume mwananchi bali wewe msaidie, masuala ya ramani ni masuala yenu ya kitaaluma na tutoke katika tabia hiyo na kwenda kusaidia wananchi" amesema Mhandisi Sanga.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Wizara hiyo hatua kali zitachukuliwa kwa watumishi wa sekta ya ardhi watakaochelewesha huduma kwa makusudi.
"Hili ni jambo tunalolipiga vita sana, ni wasihi wakuu wa Idara kukagua kazi za wasaidizi wao kama ni kazi ikipokelewa itolewe".
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi SMZ Bi Mhaza Gharib Juma amesema, Wiki ya Ardhi inayoadhimishwa itaimarisha mashirikiano baina ya Zanzibar na Tanzania Bara katika masuala ya sekta ya ardhi hasa ikizingaitiwa lengo kuu la serikali zote mbili ni kuisaidia jamiii.
Aidha, ametaka kuangalia namna sekta ya ardhi itakavyoweza kuimarisha masuala ya uwekezaji nchini kwa kuwa ardhi ni kila kitu na kusisitiza kuwekwa mikakati imara itakayoweza kutumia ardhi kwa uadilifu na haki ili kuimarisha uwekezaji na kupata fedha zitakazoongeza huduma mbalimbali kwa jamii.
Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi inaadhimisha Wiki ya Ardhi kuanzia tarehe 2 hadi 5 Desemba 2024 ambapo mbali mambo mengine wiki hiyo inatumika kujadili utoaji huduma za kisekta pamoja na uwepo mawasilisho mbalimbali kwa lengo la kufanya maboresho ya maeneo yenye changamoto.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi SMZ Bi Mhaza Gharib Juma akizungumza katika mkutano wa Maadhimisho ya Wiki ya Ardhi yanayoendelea jijini Dodoma.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Bi. Lucy Kabyemera akizungumza katika mkutano wa Maadhimisho ya Wiki ya Ardhi tarehe 2 Desemba 2024 jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi mhnadisi Anthony Sanga (kulia) na Naibu wake Bi. Lucy Kabyemera (kushoto) wakifurahia jambo na Mpima Ardhi wa kwanza mwanamke Tanzania Bi. Nina Nimwesigwa Rutakyamirwa wakati wa mkutano wa Maadhimisho ya Wiki ya Ardhi yanayofanyika jijini Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi mhnadisi Anthony Sanga (aliyekaa kati kati) pamoja na viongozi wengine wakiwa katika picha ya pamoja na wasajili wa Hati pamoja na wale wa Mabaraza ya Ardhi na Nyumba ya wilaya wakati wa mkutano wa Maadhimisho ya Wiki ya Ardhi yanayofanyika jijini Dodoma.
( PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
Social Plugin