Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
MKUU wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Ali Mohamed Shein, amewataka wahitimu wa chuo hicho kutochagua kazi wanapoingia katika soko la ajira, huku akiwakumbusha kwamba mafanikio yao kielimu yanaakisi uwezo na nafasi yao ya kufanikiwa kimaisha hata katika mifumo isiyo rasmi ya ajira.
Hayo yamesemwa na Rais Mstaafu wa Zanzibar na Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe , Dkt. Ali Mohamed Shein wakati wa Mahafali ya 23 ya Chuo Kikuu Mzumbe, Kampasi ya Dar es Salaam, yaliyofanyika leo Desemba 5, 2024 katika Kituo Cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mahafi hayo, Dkt. Shein amesema kusoma ni njia moja katika kutafuta maisha, na kwamba hakuna njia ya mkato katika mchakato huo, huku akiwapongeza kwa mafanikio waliyoyapata katika hatua hiyo kielimu na kuwatakia kila la kheiri wanapoingia katika hatua ya tatu ya ushindani kwenye soko la ajira.
“Kusoma ni njia miongoni mwa njia katika kutafuta maisha na katika hilo hakuna njia ya mkato, nyie mshavuka katika hatua ya kwanza na ya pili kielimu na sasa mnaingia hatua ya tatu. Elimu haina mwisho, leo nawapongeza kwa juhudi kubwa, mmehangaika kusoma na hatimaye mmeweza.
“Jitihada kubwa mmeonesha kuwa mnaweza kujipambania na hiyo ni uthibitisho kwamba mnaweza kujipambania nje ya vyuo, manweza kujipambania katika soko la ushindani wa ajira, wito wangu kwenu ni kwamba msichague kazi, msisubiri kuajiriwa serikalini, tumieni elimu kujiajiri.
“Kuhitimu kwenu chuo, ni mwanzo wa mitihani ya maisha, kwahiyo jiandaeni vema na mitihaani hiyo, mkawe na kiu na hamu kubwa ya kutaka kusonga mbele kwa mafanikio, huu ni ushauri saw ana nilioutoa kwa wahitimu wa Mbeya na Morogoro.
“Soko la ajira lina ushindani mkubwa, mjitahidi kutafuta ajira, ila kumbukeni hili mlilosikia kuwa mtu aliyehitimu chuo 1995, hakupata ajira, lakini akachagua kujiajiri Sekta ya Ufugaji, akachagua afuge kuku, kuliko kukaa bure kusubiri ajira ya serikalini na kimsingi ufugaji wa kuku una tija kubwa.
“Na akaifanya hiyo kazi ndani ya maisha yake, kwa hiyo msichague kazi, kazi yoyote nzuri itakupa matokeo na siamini kwamba kuna kazi mbaya za kutafuta maisha. Kwa hiyo msipoteze muda wowote wa kutafuta kazi serikalini, sio lazima muajiriwe, jipangeni kujiajiri pia.” Ameeleza Dkt. Shein
Katika hotuba yake kwenye mahafali hayo, Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Saida Yahya-Othman, amewapongeza wafanyakazi wa chuo kwa kazi kubwa na adhimu wanayoendelea kuifanya ya kuwaandaa vijana, na kwamba anaamini wanaohitimu hao wako tayari kuikabili dunia na changamoto zake.
Prof. Saida amesema “Niwapongeze wahitimu wote mtakaotunukiwa Stashahada, Astashahada na Shahada leo, juhudi na uvumilivu mliouonesha kipindi chote cha masomo yenu, hakika zinawastahilisha vyeti mnavyopokea leo.
“Tunaposherehekea mafanikio ya kuhitimu masomo yetu, tufanye tafakuri ya maisha yetu ya chuoni na yale ya baadae, na changamoto zitazotukabili katika soko la ajira, na katika maisha yetu kwa ujumla. Changamoto ni nyingi, na zimeathiri kwa kiasi kikubwa mfumo wa kiutendaji na ajira.
“Tukumbuke huu ndiyo mwanzo wa elimu yetu ya ulimwengu. Wale waliowahi kupata barua pepe kutoka kwangu, watakuwa wameiona nukuu ya Mwalimu Nyerere mwisho wa kila ujumbe wangu isemayo: “A man stops himself from thinking if he assumes that anyone exists who cannot teach him something.”
“Kutunukiwa kwetu shahada, hata kama ya uzamivu, isitufanye kufikiri kuwa tunajua yote, au hata kuwa tunajua mengi, kwani kwenye dunia ya leo, kila tujuacho ni tone baharini. Na ulimwengu una mengi ya kutufundisha nje ya darasa. Tusimdharau yeyote kuwa hajui.
“Tusi kubwa tunaloweza kulitoa kwa mwenzetu ni ‘Anajua nini yule!’ Anajua. Inawezekana hajui unayojua wewe, lakini anajua kitu ambacho wewe hukijui. Kila mtu ana maarifa ambayo wengine hawana. Jukumu letu ni kujaribu kujifunza kile akijuacho. Tusidharau ujuzi wa mtu kwa sababu tu hajaelimika kishule,” aliosema Prof. Saida.
Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Ali Mohamed Shein, akiwatunuku vyeti akiwatunuku vyeti wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo yao. Vyeti hivyo vimetolewa leo Desemba 05, 2024 wakati wa Mahafali ya 23 ya Chuo Kikuu Mzumbe yaliyofanyika katika Kituo Cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Dkt. Ali Mohamed Shein, akizungumza wakati wa Mahafali ya 23 ya Chuo Kikuu Mzumbe yaliyofanyika katika Kituo Cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam leo Novemba 05, 2024.
Matukio mbalimbali katika wakati wa Mahafali ya 23 ya Chuo Kikuu Mzumbe yaliyofanyika katika Kituo Cha Mikutano cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam leo Desemba 05, 2025.
Social Plugin