Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MSIGWA AKABIDHIWA OFISI YA MSEMAJI MKUU WA SERIKALI, AAHIDI KUFANYA KAZI KWA KUKIDHI MATARAJIO YA RAIS SAMIA




Na Dotto Kwilasa, DODOMA

KATIBU Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Idara ya Habari - Maelezo, Bw. Gerson Msigwa, amekabidhiwa rasmi Ofisi hiyo huku akiahidi kutekeleza majukumu yake kwa kujitolea na kwa lengo la kukidhi matarajio ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Msigwa amechukua nafasi hiyo kutoka kwa aliyekuwa Msemaji Mkuu wa Serikali, Balozi Thobias Makoba, ambaye amepangiwa majukumu ya kuiwakilisha Tanzania kimataifa kama Balozi.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo yaliyofanyika leo, Desemba 13, 2024, Jijini Dodoma, Msigwa alisema, "Nimeambiwa baadhi ya masuala mbalimbali ya waandishi wa habari bado yanahitaji kufanyiwa kazi, naahidi kuyashughulikia kwa nguvu kubwa. Ninachoomba ni ushirikiano wenu."

Pia, Msigwa aliwashukuru waandishi wa habari kwa namna wanavyotekeleza majukumu yao kwa weledi na nguvu, na kuahidi kuwa baada ya Sikukuu za mwisho wa mwaka atakutana nao ili kujadili na kupanga mikakati ya kufanya kazi kwa umoja kwa maslahi ya Taifa.

"Nawashukuru viongozi wanaoondoka wanaoniachia kijiti kwa kazi kubwa waliyoifanya. Idara ya Habari - MAELEZO niliyoiacha ni tofauti na ninayoikuta, naahidi na naamini tutasonga mbele zaidi," alieleza.
Aidha, Msigwa amefafanua kuwa, tarehe 19 Desemba, 2024, Jijini Dar es Salaam, atatoa taarifa yake ya kwanza kama Msemaji Mkuu wa Serikali. "Tutazungumza mengi siku hiyo yanayohusu maendeleo ya Taifa letu. Waandishi wa habari tuungane kwa pamoja kuwapa Watanzania taarifa za nchi yetu," alisisitiza.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nicholaus Mkapa, amewakilisha uongozi na wafanyakazi wote wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa kutoa shukurani kwa viongozi na wafanyakazi wa Idara ya Habari - MAELEZO kwa ushirikiano wao mkubwa katika ujenzi wa Taifa.

"Tunaikabidhi Idara ya Habari - MAELEZO kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwenda Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, ikiwa na Taasisi zake tatu; Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), na Bodi ya Ithibati," alisema.

Naye, aliyekuwa Msemaji Mkuu wa Serikali, Balozi Thobias Makoba, alitoa shukurani kwa waandishi wa habari kwa ushirikiano wao mkubwa na kwa kazi waliyoifanya pamoja.

 "Nawashukuru sana waandishi wa habari kwa kipindi tulichofanya kazi pamoja na kwa ushirikiano, mmekuwa wazalendo katika utekelezaji wa majukumu yenu," alisisitiza, akitolea mfano wa namna waandishi walivyokesha pamoja wakati wa tukio la ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa Kariakoo.

Balozi Makoba pia ametumia nafasi hiyo kushukuru Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwa ushirikiano wa pamoja, kutoka kwa viongozi hadi wafanyakazi wa ngazi zote.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com