PROFESA PIUS YANDA AELEZEA MCHANGO WA UHANDISI JENI NA BIOTEKNOLOJIA KATIKA KUKABILIANA NA MABADILIKO YA TABIA NCHI


MTAALAMU wa masuala ya mabadiliko ya tabia nchi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Pius Yanda amesema kuwa uhandisi jeni kitaalamu biotechnology ina mchango mkubwa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kupunguza kasi ya uzalishaji wa hewa ukaa.

Alishauri watafiti wajengewe uwezo katika kutafiti kuhusu bunifu ambazo zitasaidia katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Profesa Yanda kutoka Taasisi ya usimamizi wa maliasili, mazingira na mabadiliko ya tabia nchi aliyasema hayo jana wakati akitoa mada katika Kongamano na maonyesho ya tisa ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu yaliyoandaliwa na Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).

Katika mada yake kuhusu mchango wa sayansi, teknolojia na ubunifu katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kuongeza uhandisi jeni, alisema teknolojia hiyo imeanza kutumika kwa kiasi kidogo na sababu ni kutokuwa na teknolojia ya kutosha kuitumia.

Alisema Tanzania ina misitu mingi na maliasili nyingi ambazo ni malighafi muhimu kutumika kwenye uhandisi jeni.

"Uhandisi jeni unatumika kwenye maeneo mengi ikiwemo elimu, afya, kilimo na maeneo mengine hivyo kuna kila sababu ya kuhakikisha kuna ubunifu wa ziada kutumia teknolojia hii kwa kiasi kikubwa," alisema Profesa Yanda.

Pia alieleza kuwa kuna fursa nyingi za kutumia teknolojia hiyo.

Profesa Yanda alisema kwa kushirikiana na nchi zilizoendelea hususan katika utafiti, wanaweza kuwa na ubunifu bora zaidi wa matumizi ya uhandisi jeni kwa maendeleo ya Tanzania.

Alisema ubunifu wa ziada unahitajika ili kutumia rasilimali zilizopo kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

"Mabadiliko ya tabia nchi yanatuathiri zaidi Afrika na Tanzania hivyo, suala la kutumia b'ayoteknolojia kwa ajili ya kutengeneza uchumi, ni vema kuboresha ikolojia kwa kuboresha maisha ya watu, kipato na kuchangia uchumi wa nchi," alieleza.

Aliongeza kuwa kwa kujikita katika teknolojia hiyo, Tanzania itanufaika na kupata maendeleo.

Kuhusu matumizi ya nishati safi, Profesa Yanda alisema Tanzania itakuwa mstari wa mbele katika matumizi ya nishati hiyo kwa kuhakikisha jamii inayoishi vijijini waweze kushiriki katika mkakati huo.

Alisema utashi wa kisiasa unaoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan unaibeba Tanzania kuwa mstari wa mbele katika kuongeza matumizi ya nishati safi na kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post