Na Dotto Kwilasa, Dodoma
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora George Simbachawene amesema Ofisi yake imeendelea kupokea malalamiko ya watumishi wanaokataliwa kupokelewa katika vituo wanavyohamishiwa au kuajiriwa.
Hayo ameyasema leo jijini hapa wakati akifungua kikao Kazi cha Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma ambapo ameeleza upendeleo wa fursa mbalimbali za kiutumishi, kutumia utashi binafsi katika kutafsiri Miongozo inayosimamia haki za watumishi, unyanyasaji wa kijinsia, na ucheleweshaji wa haki na stahiki za kiutumishi ni malalamiko yaliofika ofisi kwake.
"Baadhi ya mambo hayo ni kwa Waajiri kuchagua aina ya watu wa kufanya nao kazi, kutopokea, kukataa na kuficha barua zenye maelekezo mahsusi ikiwemo barua za uhamisho (kuhamia na kuhama). Ninyi mliopo humu ndio washauri wakuu wa Waajiri wenu, " Amesema
Na kuongeza "Haya yanayofanyika ni kinyume cha utaratibu na ni utovu wa nidhamu, na halivumiliki endapo kweli tunataka kujenga utumishi wa umma na hapa nitoe melekezo kwa utaratibu huu mpya uachwe kwa kuwa kinachofanyika ni kinyume na utaratibu, "Amesema.
Aidha ameendelee kusisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili kwa kuwa tumeendelea kupokea malalamiko kuhusu vitendo vya uvunjifu wa maadili ikiwemo Rushwa, lugha zisizofaa, kufanya udanganyifu wa nyaraka ikiwemo kughushi barua za masuala mbalimbali ya kiutumishi kama uhamisho wa kwenda sehemu za mijini na zenye maslahi mazuri.
" Hivyo, nitoe wito kwa wote wanaojihusisha na tabia hiyo kuacha mara moja na kwa taasisi ambazo watumishi wake wamebainika kuwa na mapungufu yaliyoainishwa, Mamlaka ya Nidhamu ya watumishi katika Taasisi hizo ichukue hatua stahiki dhidi ya watumishi hao kwa mujibu wa taratibu za Utumishi wa Umma na ningependa kupata taarifa kuhusu namna walivyoshughulikia masuala hayo na kuyahitimisha, " Amesema
Na kuendelea kusema "Ninatambua kuwa wajibu wa Watumishi wa Umma unaendana na haki zao Kwa kutambua hilo, katika bajeti ya mwaka 2023/2024 Serikali kupitia Ofisi hii imewapandisha vyeo watumishi 229,159 na kuwabadilisha Kada Watumishi 9,654,"
Vilevile amesema, Serikali imetoa nyongeza ya mwaka ya mshahara kwa watumishi wake na itaendelea kuboresha maslahi ya watumishi kulingana na uwezo wa uchumi.
Ni jukumu lenu kama wasimamizi wa watumishi wa Umma kuendelea kuwasimamia watumishi walio chini yenu kwa kuwaelimisha kuhusu haki na wajibu wao ili wanapodai haki wajue kuwa kuna wajibu wanapaswa kuwa wametekeleza.
Amesema Serikali kwa kutambua kuwa Rasilimaliwatu ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya Taifa imekuwa ikitoa vibali vya Ajira kwa Kada mbalimbali. Katika mwaka wa Fedha 2024/2025 Serikali imetoa kibali cha kuajiri watumishi arobaini na tano elfu na themanini (45,080) wa kada mbalimbali, kati yake watumishi elfu kumi mia tatu tisini na sita (10,396) ni wa Kada za Afya, watumishi elfu kumi mia tano tisini (10,590) wa kada za Ualimu na Watumishi elfu ishirini na nne na tisini na nne (24,094) wa Kada nyingine.
" Ningependa kuzungumzia tena suala la kukaimu nafasi za uongozi na ujazaji wa nafasi hizo Katika eneo hili bado kuna changamoto mbalimbali ambazo ni pamoja na kuendelea kukaimisha maafisa wasio na sifa za kuteuliwa, kuchelewa kuwaombea vibali vya kukaimu na kulipwa posho ya kukaimu, Maafisa kukaimishwa nafasi hizo kwa muda mrefu pasipo kuanzisha mchakato wa ujazaji wa nafasi, kutoteua watumishi ambao mchakato wao wa uteuzi umekamilika.
Hali hii inasabisha malalamiko mengi kwa watumishi hao na ongezeko la madeni kwa Serikali Ukifuatilia kwa undani unabaini kuwa wenye jukumu hili ambao ni nyie nyote mliopo hapa hamjawajibika ipasavyo.
Hivyo, Kupitia kikao hiki naelekeza kila mmoja wenu kufanyia kazi changamoto zote zilizobainishwa kwenye eneo la kukaimu nafasi za uongozi pamoja na ujazaji wa nafasi hizo kwa wakati.
Aidha, kupitia kikao hiki nitoe tahadhari kwa wasimamizi wa kazi mahala pa kazi ambao hawatatekeleza majukumu yao ipasavyo hatutasita kuchukua hatua stahiki.
Social Plugin