Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WIZARA YA MADINI YAAHIDI KUHARAKISHA USAJILI WA BODI YA WANAJIOLOJIA TANZANIA

Na Hadija Bagasha Tanga,

WIZARA ya Madini imesema  itahakikisha inaharakisha mchakato wa kusajili bodi ya wanajiologia ili kusaidia kuongeza tafiti  na tambuzi kwenye kazi za kijiolojia  ndani na nje ya nchi sambamba na kufikia malengo ya wizara hiyo ifikapo 2030.


Wataalamu hao wamekutana kwenye mkutano wao  mkuu wa kila mwaka ulioshirikisha wanajiolojia kutoka ndani na nje ya nchi na kufanyika jijimi Tanga ambapo pamoja na mambo mengine wakajadili  mustakabali wa madini ya kimkakati nchini Tanzania.

Akizungumza katika Mkutano huo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya madini Dkt. Msafiri Mbibo amesema kwamba amelipokea jambo hilo huku akisema wizara hiyo itahakikisha uundwaji wa bodi hiyo unafanyika kwa haraka.


Hatua hiyo inatokana na kauli iliyotolewa kwenye mkutano na Rais wa Jumuiya wa Wanajiolojia Tanzania Dkt Elisante Mshiu ambapo alisema kwamba kama taasisi hiyo haitopata bodi basi kunaweza kuwa kikwazo katika mchango wao kuweza kutimiza maono ya 2030.

Naibu Katibu Mkuu alisema kwamba wamelipokea  na wataendelea kuwasiliana kuona jinsi ambavyo wanaweza kuharakisha uundwaji wa bodi hiyo ili kuchochea kasi ya ukuaji wa chombo chao.


“Wizara  ya madini imeendelea  kutumia wanajiosayansi katika kufanya tafiti kwa lengo la kubaini uwepo wa madini nchini kupitia maono ya Vision 2030 madini ni maisha,madini ni utajiri ni lengo la wizara ya madini na maono ya mheshimiwa Waziri kuhakikisha kwamba maisha ya watanzania yanabadilishwa kutokana na rasilimali hizi ambazo ni za thamani sana zilizopo Nchini,”alibainisha Katibu Mkuu.


‘Ili kufanikisha maono haya wanajiosayansi wameendelea kutumia utaalamu wao kkatika kufanya utafiti wa kina wa jiofizikia kwa kutumia teknolojia ya kisasa kwa lengo la kutambua tabia za miamba utambuzi huu unatuwezesha kufanyika kwa tafiti nyingine za jiosayansi zenye kuwezesha kubaini aina mbalimbali za madini yanayopatikana nchini,”alisisitiza Katibu Mkuu huyo.


Kwa upande wake Rais wa jumuiya ya wanajiolojia Tanzania Dkt. Elisante Mshiu amesema kwamba wamekutana kwajili ya kujadiliana juu ya mabadiliko kutoka kwenye nishati chafuzi kwenda kwenye nishati salama ambazo zote ukiangalia ni malengo ya serikali.


Amewataka wanajiolojia kuelewa majukumu yao hususani katika kuelekea kwenye maono ya 2030 huku akieleza kwamba bila kuwa na bodi ya usajili ya wanajiosayansi maono ya 2030 yanaweza kuwa na changamoto hivyo ameendelea kusisitiza umuhimu wa uundwaji bodi hiyo.


“Kupitia Wizara ya madini tayari kuna juhudi kubwa zinafanyika na hatua hizo ziko mwishoni lakini ujumbe wetu kwa serikali ni kupeleka jambo hili kwa haraka ili liendane na kasi ya serikali kimaendeleo wito wangu kwa watanzania ni kwamba madini ni utajiri na nchi yetu ni tajiri kirasilimali tuko hapa hapa kuhakikisha tunaisaidia serikali kufikia malengo iliyojiwekea,”alisema Rais Mshiu.

 

Naye afisa uhusiano kutoka kampuni ya Geofield Tanzania Stephen Goroi ameipongeza serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mazingira mazuri kwa kampuni za wawekezaji wa kuweza kufanya kazi katika mazingira mazuri ikiwa ni pamoja na kushawishi wawezkezaji wa nje kuja kuwekeza nchini Tanzania.


“Wanapokuja wawekezaji wengi kuwekeza nchini mwetu sisi kampuni za kitanzania  tunaofanya kazi za utafiti na uchorongaji  zinapata nafasi ya kufanya kazi za uchimbaji na utafiti kwenye maeneo mbalimbali ya migodi nchini Tanzania,”alisisitiza Goroi.


Wanajiosayansi kutoka ndani na nje ya nchi ya tanzania wamekutana  jijini Tanga kwa ajili ya mkutano wao wa mwaka TGS 2024) wenye  lengo la kuwezesha wanajiosayansi kupeana taarifa za kitaalamu kubadilishana uzoefu na kujadili masuala yanayohusu utafutaji na uendeshaji wa rasilimali za madini,mafuta,gesi asilia,maji na joto la ardhi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com