Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI KUTATUA CHANGAMOTO ZINAZOKIKABILI CHUO CHA SERIKALI ZA MITAA




Na Dotto Kwilasa, Dodoma

Chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI) kilichopo Hombolo, mkoani Dodoma, kimefanya mahafali yake ya 16, huku kikiwa kinakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazokwamisha baadhi ya shughuli za maendeleo yake.

Mahafali hayo yaliyofanyika December 5,2024 yameshirikisha wahitimu kutoka idara mbalimbali za chuo hicho, ambao wamehitimu mafunzo ya juu katika masuala ya usimamizi wa Serikali za Mitaa.

LGTI kinakabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa wataalam katika maeneo mbalimbali na kuhatarisha ufanisi wa chuo hicho katika kutoa mafunzo bora na ya kisasa kwa wahitimu wake.

Aidha, miundombinu ya barabara inayozunguka chuo hicho imekuwa katika hali mbaya, ikiwalazimu wahitimu na wahadhiri kukumbana na ugumu wa usafiri, jambo linalozua vikwazo kwa usafirishaji wa vifaa na huduma nyingine muhimu kwa ustawi wa chuo.

Hali hiyo imewaibua viongozi wa Chuo hicho ambapo wameiomba Serikali kufanya jitihada za haraka ili kuboresha miundombinu ya barabara na kuongeza rasilimali watu katika chuo hicho, ili kiweze kutimiza jukumu lake la kutoa elimu bora kwa wanafunzi wa serikali za mitaa.

Kutokana na hayo Naibu Waziri wa TAMISEMI, Dkt.Festo Dugange, amesema chuo hicho kina nafasi muhimu katika kusaidia serikali kuzitatua changamoto hizo kupitia utafiti, mafunzo, na ushauri wa kitaalamu.
Dkt. Dugange amesema chuo hicho kimekuwa kikijenga uwezo wa wataalamu wanaoweza kusaidia serikali kubuni miradi ya kimkakati yenye tija.

Amesisitiza kuwa halmashauri zinapaswa kuibua miradi inayoendana na mahitaji ya maeneo yao badala ya kuiga miradi kutoka halmashauri nyingine.

"Baadhi ya halmashauri kunaanzisha miradi ya stendi za mabasi bila kuzingatia mahitaji halisi ya kiuchumi na kijamii ya maeneo yao, hatua hiyo imekuwa changamoto kwani baadhi ya halmashauri hazihitaji miradi mikubwa ya aina hiyo, " amesema

Dkt. Dugange amehimiza chuo hicho kuendelea kutoa mafunzo na kuwajengea uwezo wataalamu wa serikali za mitaa ili waweze kusimamia miradi kwa ubunifu na weledi na kupongeza mafanikio ya kubuni miradi yenye tija katika halmashauri mbalimbali nchini.

Pamoja na hayo Naibu Waziri huyo amekitaka Chuo cha Serikali za Mitaa (LGTI) Hombolo kuhakikisha matokeo ya tafiti yanatumika kutatua changamoto zinazozikabili halmashauri badala ya kubaki kwenye makabati.

"Tafiti nyingi zimekuwa zikifanyika lakini hazitumiki ipasavyo katika kutatua matatizo hivyo ni wakati wa wanazuoni wa Hombolo kushirikiana na halmashauri kutatua changamoto zilizopo ,ni jukumu la wanazuoni wa Hombolo kupeleka maarifa haya kwenye halmashauri na kutatua changamoto kwa vitendo, badala ya kufungia tafiti kwenye makabati,” amesema Dkt. Dugange.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com