Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limewataka wawekezaji, wazalishaji na wafanyabiashara mkoani Pwani kusajili majengo yanayotumika kuuza na kuhifadhia bidhaa za Chakula na vipodozi na wale wenye viwanda wahakikishe wanathibitisha ubora bidhaa zao kabla ya kwenda sokoni.
Rai hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Meneja Kanda ya Mashariki TBS Bi. Noor Meghji kwenye Maonesho ya Viwanda na Uwekezaji yaliyofanyika mkoani humo.
Aidha, aliwataka wazalishaji wadogo wadogo nao kuthibitisha bidhaa zao, kwani Serikali kupitia TBS inatoa huduma ya uthibitishaji wa bidhaa kwa wajasiriamali bure na kinachotakiwa ni wao kutambuliwa na SIDO .
"SIDO ni taasisi mama inayohudumia wazalishaji wadogo, basi itakapokutambulisha kwetu huduma ya uthibitishaji wa bidhaa hiyo unakuwa ni bure, kwa hiyo hakuna sababu yoyote ya kupeleka bidhaa sokoni bila kuwa na nembo ya ubora," alisema Meghji.
Alipongeza jitihada ambazo zimefanywa na mkuu wa mkoa wa Pwani kufanikisha maonesho hayo na kwamba TBS imeshiriki ili kuwahimiza washiriki wa maonesho hayo kuzingatia ubora bidhaa wanazozalisha.
"Iwepo haujathitibisha ubora wa bidhaa unazozalisha, haujathibitisha ubora wa mifumo basi biashara na uwekezaji huo hauwezi kuwa endelevu," alisema.
Alitumia fursa hiyo kuwaeleza washiriki wa maonesho hayo majukumu ya shirika hilo na huduma zinazotolewa na TBS.
Meghji alisema majukumu ya TBS ni kuhamasisha masuala ya viwango, kufanya uthibitishaji wa bidhaa pamoja na mifumo, kuezeshaji upimaji wa bidhaa husika,kufanya ukaguzi maeneo mbalimbali yanahusika na uuzaji na usambazaji wa bidhaa.
Mengine ni kusimamia bidhaa zinazoingia nchini kuhakikisha ni zile zenye ubora na salama ndizo zinazoingia nchini kwa kufanya ukaguzi wa bidhaa kabla ya kuingia nchini.
Aidha, Meghji alisema TBS inatoa huduma za kimaabara ambapo shirika hilo lina maabara tisa ambazo zinahusisha upimaji bidhaa mbalimbali.
"Lakini pia tunatoa huduma ya upimaji binafisi kwa wanaohitaji huduma hii, kwa mfano mzalishaji yeyote anayetaka kuuza nje ya nchi kuna huduma TBS tunatoa kuwezesha wazalishaji kusafirisha bidhaa zao kwenda nje.
TBS tuna huduma pale mzalishaji anapotaka kusafirisha bidhaa zake kwenda nchi yeyote ili uweze kujua je katika nchi hiyo kuna mahitaji gani yanatakiwa, kwa hiyo ukija TBS utapata huduma hiyo," alisema Meghji na kuongeza;
"Unaweza kuwa unataka kupeleka bidhaa nje ya nchi ukaabiwa tunataka bidhaa hiyo iwe imetambuliwa na taasisi kutoka nchi yako ambayo inathibitisha ubora na usalama wa bidhaa hiyo, basi TBS tunatoa huduma hiyo."
Social Plugin