NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM
MTANDAO wa Jinsia Tanzania (TGNP) imetoa mafunzo maalum kwa vijana kutoka vyuo mbalimbali nchini na wawakilishi wa mashirika ya vijana na kujadili mafanikio na changamoto kuelekea miaka 30 ya Azimio la Beijing, linalotarajiwa kuadhimishwa Machi 2025 jijini New York, Marekani.
Mafunzo hayo yamefanyika leo Desemba 29, 2024 jijini Dar es Salaam yakilenga kuangazia hatua zilizopigwa katika ajenda za usawa wa kijinsia, hasa kwa mtoto wa kike, na kuwashirikisha vijana kuchukua nafasi zao katika harakati hizo.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Flora Ndaba kutoka Idara ya Ujenzi wa Nguvu ya Pamoja na Harakati ya TGNP, amesema kuwa Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia mikakati kama asilimia 10 ya mapato ya halmashauri, mifuko ya uwezeshaji wanawake kiuchumi, na majukwaa ya uwezeshaji.
Hata hivyo, amebainisha changamoto kadhaa, ikiwemo uwepo wa mifuko ya kidigitali inayojulikana kama "kausha damu," ambayo badala ya kuwasaidia wanawake imekuwa mzigo.
“Tumepiga hatua katika kuwainua wanawake kiuchumi, lakini bado tunakabiliwa na changamoto za mifuko isiyo rafiki kwa wanawake,” amesema Ndaba.
Kwa upande wake, Walta Carlos, mmoja wa wawezeshaji, amesisitiza umuhimu wa kuboresha huduma za afya kwa wanawake. Amesema serikali inapaswa kuongeza vituo vya afya, vifaa tiba, na wataalamu wa afya katika maeneo mbalimbali ili kupunguza vifo vya uzazi.
“Tunaishukuru serikali kwa juhudi zake, ikiwemo programu ya kuwarudisha shuleni wasichana waliopata ujauzito, lakini bado tunahitaji mazingira bora zaidi kwa msichana na mtoto wake,” amesema Walta.
Nae Mshiriki Dady Thomas amezungumzia suala la wanawake kushiriki katika uongozi, akisema bado kuna changamoto ya wanawake wengi kujitokeza kugombea nafasi za uongozi.
“Serikali imejitahidi kutoa nafasi kwa wanawake, lakini jamii bado inaamini kuwa mwanamke hawezi kuongoza. Tunahitaji kuelimisha jamii zaidi,” amesema Thomas.
Nasra Mohammed kutoka Chuo Kikuu cha SAUT amesema kuwa mashirika yasio ya kiserikali na serikali kwa ujumla wamepiga hatua katika kutokomeza ukatili wa kijinsia, ingawa juhudi zaidi zinahitajika kuhakikisha tatizo hilo linatokomezwa.
Social Plugin