Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TRA SHINYANGA YAWAPONGEZA NA KUWAPA ZAWADI WAFANYABIASHARA WAZALENDO KWA KULIPA KODI KWA HIARI

Mwanasheria wa TRA kutoka Makao Makuu, Elisha Shigela (kushoto) kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda akikabidhi zawadi kwa Mkurugenzi wa Gaki Investment Co. Ltd & East Africa Spirit (T) Ltd Gasper Kileo (GAKI) kwa kuonesha mfano bora wa ulipaji kodi kwa hiari na kwa wakati
Mwanasheria wa TRA kutoka Makao Makuu, Elisha Shigela, kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda akikabidhi zawadi kwa Mkurugenzi wa Gilitu Enterprises Co. Ltd, Gilitu Makula (katikati) kwa kuonesha mfano bora wa ulipaji kodi kwa hiari na kwa wakati

Na Mwandishi Wetu, Malunde 1 blog

Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Shinyanga imewapongeza na kuwapa zawadi za shukrani baadhi ya wafanyabiashara ambao wamekuwa wazalendo kwa kulipa kodi kwa hiari, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuendeleza maendeleo ya taifa. 

Pongezi hizo zimetolewa leo, Desemba 19, 2024, na Mwanasheria wa TRA kutoka Makao Makuu, Elisha Shigela, kwa niaba ya Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda, kwa wafanyabiashara wa mfano ikiwa ni pamoja na Kampuni za Gilitu Enterprises Co. Ltd, East Africa Spirit (T) Ltd, Gaki Investment Co. Ltd, na mfanyabiashara Bi Clecensia Ernest.

Shigela amesema wafanyabiashara wanachangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya taifa na kwamba serikali inawathamini kwa juhudi zao za kulipa kodi kwa hiari. 

“Mjenga nchi ni mwananchi. Wafanyabiashara wamejua kazi yao na serikali inathamini michango yao. Mchango wao katika kulipa kodi unasaidia kuleta maendeleo ya miundombinu, elimu, afya, maji, na umeme”,amesema Shigela.

Shigela amewapongeza wafanyabiashara kwa mchango wao mkubwa na kusema, “Kila barabara inayojengwa, kila shule inayojengwa, na kila huduma ya afya inayotolewa ni matokeo ya mchango wenu mkubwa. Asanteni kwa kuwa mabalozi wa maendeleo ya taifa letu. Serikali itahakikisha inawawezesha na kuwapa huduma bora ili mtimize wajibu wenu kwa hiari”.

Katika pongezi zake, Shigela ameongeza kuwa ushirikiano kati ya serikali na wafanyabiashara ni muhimu katika kufanikisha malengo ya maendeleo. 

Elisha Shigela

“Kodi mnazolipa ni kiungo muhimu cha maendeleo ya nchi. Serikali inahitaji michango yenu ili tuweze kufikia malengo yetu ya kuleta maendeleo kwa wananchi,” amesema.

Amesisitiza kuwa TRA inaendelea kushirikiana na walipa kodi kwa kuhakikisha kila mmoja anatimiza wajibu wake kwa hiari, huku ikiendelea kutoa huduma bora na kuwapa msaada unaostahili. 

“TRA itaendelea kuhakikisha ushirikiano huu unaimarika. Hatuwezi kufikia malengo ya maendeleo bila ninyi, walipa kodi. Asanteni kwa kuwa sehemu ya mafanikio ya taifa letu”,ameongeza

Mkurugenzi wa Gilitu Enterprises Co. Ltd, Gilitu Makula, ameelezea furaha yake kwa hatua ya serikali kuondoa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika mafuta ya kupikia, ambayo ilikuwa ikiwaletea changamoto kubwa katika biashara zao. 

“Nashukuru kwa kuondolewa kwa VAT katika mafuta ya kupikia. Hii imetusaidia kulipa kodi kwa urahisi na kuelewa umuhimu wake kwa maendeleo ya nchi,” amesema Makula.

 Amesema kampuni yao imepata mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake mwaka 2017 na kwa msaada wa TRA na serikali, wameweza kushinda changamoto hizo na kuimarika sokoni. 

“Kodi tunazolipa zimetuletea maendeleo. Tunapata miundombinu bora, maji, umeme, na usalama. Tunashukuru TRA kwa ushirikiano huu na tunajivunia kulipa kodi,” ameongeza Makula.

Gaspar Kileo (GAKI)

Naye Mkurugenzi wa Gaki Investment Co. Ltd & East Africa Spirit (T) Ltd Gasper Kileo, ameishukuru TRA kwa kutambua mchango wao na kwa ushirikiano mzuri katika utendaji wa biashara.

 “Tunafurahi kuona TRA inabadilika na kuweka mkazo kwenye ushirikiano na walipa kodi. Tunashirikiana kwa amani, na changamoto zetu zinapatiwa suluhisho kwa njia ya mazungumzo,” amesema Kileo. 

Ameongeza kuwa kampuni yao imepata mafanikio makubwa kutokana na ushirikiano wa karibu na TRA, na kwamba wanajivunia kulipa kodi kwa sababu wanajua inachangia moja kwa moja katika maendeleo ya taifa.

Mfanyabiashara mwingine, Bi Clecensia Ernest, amesisitiza umuhimu wa ulipaji kodi kwa maendeleo ya miundombinu na huduma za kijamii.

 “Kupitia kodi, tunapata huduma muhimu kama shule, hospitali, na miundombinu ya barabara, maji, na umeme. Kodi tunazolipa ni msingi wa maendeleo ya jamii yetu,” amesema Bi Clecensia. 

Ameongeza kuwa wafanyabiashara wanapaswa kuona ulipaji kodi kama sehemu ya mchango wao katika kujenga taifa imara na lenye maendeleo.
 Gilitu Makula

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com