Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

VETA YAWAKUTANISHA WADAU WA UTALII, UKARIMU DODOMA KUJADILI MUSTAKABALI WA SEKTA HIYO

 
Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Alhaji Jabir Shekimweri akizungumza wakati wa kongamano la Wadau wa utalii Dodoma lililoandaliwa na VETA kanda ya Kati. 

Mkurugenzi wa Veta Kanda ya Kati Ramadhani Ali Mataka akizungumza kwenye kongamano la Wadau wa Sekta ya Ukarimu na Utalii lililoandaliwa na Ofisi ya VETA Kanda ya Kati kwa kushirikiana na chuo cha VETA Dodoma. 


NA Dotto Kwilasa,DODOMA

Watoa huduma wa sekta ya ukarimu na utalii nchini wameshauriwa kufanya mapinduzi  katika sekta hiyo ili Kuongeza Ushindani na Ubunifu katika soko la utalii. 

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Alhaji Jabir Shekimweri ameeleza hayo Jijini Dodoma kwenye kongamano la Wadau wa Sekta ya Ukarimu na Utalii lililoandaliwa na Ofisi ya VETA Kanda ya Kati kwa kushirikiana na chuo cha VETA Dodoma lengo likiwa ni kuwakutanisha wadau wa sekta ya ukarimu na utalii na chuo cha VETA Dodoma ili kujadili na kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili sekta hiyo.

Shekimweri amesema, Sekta ya utalii inakua kwa kasi na mabadiliko yanaweza kusaidia kuboresha huduma na bidhaa zinazotolewa ili kuhakikisha  shughuli za utalii zinachangia katika uhifadhi wa mazingira na kiuchumi. 

"Mabadiliko haya yanaweza kuhusisha matumizi ya nishati mbadala, kupunguza uchafuzi, na kukuza utalii endelevu ambao unahifadhi mazingira, mfano, maendeleo ya teknolojia yamewezesha sekta hii kuboresha huduma za mtandao, kama vile kutengeneza mifumo ya booking mtandaoni, kuongeza matumizi ya programu za simu kwa wateja, na kutoa huduma bora kwa wageni, "amesema.
Amesema Mabadiliko katika sekta ya ukarimu yanaweza kuboresha huduma kwa wateja kwa kutoa huduma bora, za kibinafsi, na zinazozingatia mahitaji maalum ya wageni kwa kujumuisha matumizi ya teknolojia ya kisasa, kama vile huduma za kibinafsi kupitia simu au roboti, na pia mafunzo kwa wafanyakazi ili kuimarisha ustadi wao.

"Mabadiliko katika sekta ya utalii na ukarimu yanaweza kuongeza ajira na fursa za kimaisha kwa watu wengi, hasa katika maeneo ya vijijini na maeneo ya kitalii. Kukuza sekta hii kwa njia endelevu kunaweza kusaidia kupunguza ukosefu wa ajira na kuongeza mapato kwa wananchi, "amesema

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Bahi  Rebecca Sanga ametumia jukwaa hilo kuwataka Vijana wote wanaosomea Sekta Ukarimu na watoa huduma ya ukarimu  kuhakikisha kuwa wanakuwa waaminifu,Wasafi na Wachangamfu nyakati zote wawapo katika majukumu yao kwani uaminifu siku zote unalipa.

Amesema Serikali Mkoani Dodoma imeweka usalama wa kutosha hivyo watu wanaweza kutanua biashara kwa kkufanya muda wote kwasababu usalama upo na anatarajia kuona Dodoma ikishamiri.

"Niwasihi sana ndugu zangu Tasnia yetu inahitaji ukarimu,Usafi na Uchangamfu kwa tunaowahudumia,tuna hitajika kuwa wakarimu kweli kweli kwani uaminifu na ukarimu unalipa".
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Veta Tanzania CPA Anthony Kasore amesema kuwa kwasasa wana vyuo 80 vinavyotoa mafunzo ya Ufundi katika Mikoa yote Nchini, na vipo vyuo 65 vinavyoendelea kujengwa katika mikoa hiyo vinavyojumuisha wilaya 64 .

Ametaja matarajio kuwa  ifikapo mwaka 2025 ni Veta kuwa na jumla ya vyuo 145, ili kuendana na maono ya Raisi Samia ya kuwa kila Mtanzania kuwa na ujuzi kutoka katika vyuo vya ufundi Stadi hapa Nchini.

  Mkurugenzi wa Veta Kanda ya Kati Ramadhani Ali Mataka ameeleza lengo na madhumuni ya kukutana na wadau wa sekta ya Ukarimu na Utalii mkoa wa Dodoma ni kuona namna gani bora ya kutatua changamoto zinazoikabiki sekta hii kwani Dodoma ni mji Mkuu na watu wengi wanaingia kila siku. 

Licha ya hayo Mataka amesema kuwa  VETA kinaendelea kutoa mafunzo yanayokidhi viwango ili kuendana na soko la Dunia hasa katika Sekta hii ya Ukarimu.

"Dodoma, ikiwa ni kitovu cha shughuli za Serikali sasa inakua kwa kasi kubwa kiuchumi na kijamii, ambapo ukuaji huo unaibua fursa nyingi katika sekta mbalimbali, mojawapo ikiwa ni Sekta ya Ukarimu na Utalii, " amesema

Ameongeza kuwa ushirikiano wa VETA na wadau kutoka sehemu za kazi katika mafunzo utasaidia kukuza umahiri wa wanafunzi na hatimaye kupata wahitimu wenye stadi bora ambao watatoa huduma zenye kiwango cha kimataifa katika sekta ya ukarimu na utalii.

"Nitoe rai kwa wadau wa ukarimu na utalii kushirikiana na VETA Dodoma katika kutafuta fursa za kibiashara pamoja na kutatua changamoto zinazolalamikiwa katika sekta hiyo,ningefurahi kuona wadau wa sekta ya utalii wanabadilishana uzoefu na VETA katika kuwanoa vijana wanaohudumia wageni wanaoingia na kutoka katika jiji la Dodoma, "amesema Mataka.






Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com